1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi watawanya waandamanaji wa Kikurdi Kolon

Sekione Kitojo
28 Januari 2018

Polisi  ya Ujerumani  imewatawanya waandamaji wa  Kikurdi  mjini Kolon jana Jumamosi, baada ya kiasi  ya  Wakurdi 15,000 kuingia mitaani  kuandamana  kupinga mashambulizi  ya  Uturuki  kaskazini mwa  Syria.

https://p.dw.com/p/2reK3
Deutschland | Polizei löst Kurden-Demo in Köln
Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Polisi  imesema imewatawanya  waandamanaji kutokana  na  kuwapo  kwa  mabango  katika  kundi  la waandamanaji  linaloonesha  nembo  ya  chama  cha  wafanyakazi wa  Kikurdi PKK , ambazo  zimepigwa  marufuku  nchini  Ujerumani.

Maandamano  hayo  yalitayarishwa  na  NAV-DEM , chama  cha Wakurdi  ambacho  kinaelezwa  kuwa  karibu  na  chama kilichopigwa  marufuku  cha  PKK, ambacho  kimepigwa  marufuku pia  nchini  Uturuki  pamoja  na  washirika  wake  wa  mataifa  ya magharibi  kuwa  ni  kundi  la  kigaidi.

Deutschland | Polizei löst Kurden-Demo in Köln
Maandamano ya Wakurdi mjini KolonPicha: picture-alliance/Geisler-Fotopress/C. Hardt

"Idadi  kubwa  ya  waandamanaji  walishika  mabango  yenye  picha ya  kiongozi  wa  PKK  aliyeko  kifungongo Abdullah Ocalan," msemaji  wa  polisi  mjini  Kolon  aliliambia  shirika  la  habari  la AFP.

Watu  wawili walikamatwa  katika  maandamano  hayo, ambayo yamekuja  wiki  moja  baada  ya  vikosi  maalum  vya  jeshi  la Uturuki  pamoja  na  waasi  ambao  ni  washirika  wa Uturuki  nchini Syria  kufanya  mashambulizi  wakiwalenga  wanamgambo  wa Kikurdi  wa  kundi  la   vikosi  vya  ulinzi  wa  umma YPG, kaskazini mwa  Syria.

Hali  ilishakuwa  mbaya  wakati  maandamano  hayo  yalipoanza majira  ya  asubuhi  katika  mji  huo  wa  magharibi  mwa  Ujerumani, ambapo  zaidi  ya  polisi 2,000 walipowekwa  kulinda  maandamano hayo.

Deutschland | Polizei löst Kurden-Demo in Köln
Polisi wakiwakamata baadhi ya waandamanaji Picha: picture-alliance/dpa/M. Becker

"Uhuru  kwa  Wakurdi"  na "oneni  aibu, Ulaya !" yameandikwa baadhi  ya  mabango  waliyokuwa  wamebeba  waandanaji.

Polisi  waliwazuwia  waandamanaji  karibu  ya  kufikia  nusu  ya safari  yao  kuhusiana  na  nembo  za  PKK  na  kuwasindikiza kuelekea  walikoanzia.

Hakuna tukio  baya lililotokea

Hakuna  tukio  lililoripotiwa  mara  moja, lakini "hali iliendelea  kuwa tete," alisema  msemaji  wa  polisi, na  kuongeza  kwamba  alikuwa na  wasi  wasi  juu  ya  mapambano  kati  ya  waandamanaji  na polisi , ama Waturuki  wenye  msimamo  wa  kizalendo , wakati giza litakapoingia.

Ujerumani  wanaishi  kiasi  ya  Wakurdi  milioni  moja  na  watu milioni  3  wenye  asili  ya  Uturuki, na  maafisa  wameonya  dhidi  ya mivutano  baina  ya  jamii  hizo  mbili.

Deutschland Kurden-Demo in Köln
Baadhi ya picha za kiongozi aliyeko kifungoni Abdullah OcalanPicha: DW/C. Winter

Mapambano  yalitokea  kati  ya  watu  kutoka  makundi  hayo  mawili tangu  pale  Uturuki  ilipoanzisha  mashambulizi  yake  yaliyopewa jina  la "tawi la  mzaituni" ambapo  misikiti  mingi  ya  Waturuki  nchini Ujerumani  imekumbwa  na  matukio  ya  uharibifu.

"Uturuki imeanzisha  vita  vya  kimabavu  ambavyo  vinavuka mipaka  ya sheria  za  kimataifa,"  kiongozi  mwenza  wa  jamii  ya Wakurdi Mehmet Tanriverdi  aliliambia  gazeti la  kanda  la Heilbronner Stimme  jana  Jumamosi.

Deutschland Kurden-Demo in Köln
Waandamanaji wa Kikurdi wakiwa na bendera na nembo za chama cha PKKPicha: DW/C. Winter

Mara nyingi wakielezwa  kuwa  ni  idadi  kubwa  ya  watu  wasio  na taifa , Wakurdi wamekuwa  washirika  muhimu  katika  mapambano dhidi  ya  kundi  linalojiita  Dola  la  Kiislamu, lakini  baada  ya mashambulizi  ya  hivi  karibuni  ya  Uturuki wengi  waliokuwa wakitafuta  malipo wameachwa  wakiwa  wamevunjika  moyo  sana. Kumekuwa  pia  na  maandamano  madogo  ya kuunga  mkono Wakurdi  nchini  Ufaransa  jana  Jumamosi, ambapo mamia  kadhaa ya  watu  waliandamana  mjini  Paris  na  karibu  watu  500 waliandamana  mjini  Marseille.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Isacc Gamba