1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ujerumani yatoa maelezo kuhusu mshukiwa wa Berlin

22 Desemba 2016

Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari nchini Ujerumani zinaarifu kugunduliwa kwa alama za vidole za mtuhumiwa namba moja wa shambulizi la kigaidi katika soko la Krismas la mjini Berlin, Anis Amri

https://p.dw.com/p/2UkXI
Deutschland LKW nach dem Anschlag am Breitscheidplatz in Berlin
Picha: Reuters/H. Hanschke

Alama hizo za vidole zilizoonekana kwenye mlango wa lori aliloendesha na kuvamia soko la Krismas la mjini humo, na kusababisha mauaji ya watu 12 na wengine kujeruhiwa vibaya. Hatua hii inaarifiwa wakati ambapo msako dhidi ya mhamiaji huo ukiendelea nchini kote.

Gazeti la kila siku la Sueddeutsche Zeitung na vituo vya redio vya NDR na WDR vimeripoti leo hii kwamba alama za vidole za Amri zimeonekana kwenye mlango wa lori hilo. Gazeti la kila siku la Berliner Zeitung limeripoti kwamba alama za vidole za mtuhumiwa huyo zimeonekana kwenye usukani wa gari. Hata hivyo vyombo hivyo vyote havikumtaja mtoa habari hizo.

Waendesha mashtaka wa serikali wanaoongoza uchunguzi wa tukio hilo hawaupatikana mara moja kuzungumzia taarifa hizo. Awali vitambulisho vya Amri vilipatikana chini ya kiti cha lori hilo na vilionyesha Amri alibadilisha angalau mara sita majina yake na uraia wa nchi tatu tofauti.

 

Deutschland Sicherheitsmaßnahmen Weihnachtmarkt am Breitscheidplatz
Polisi wakiendeleza doria kwenye soko la Krismas la BerlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Aidha, polisi wamevamia maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na eneo wanapoishi wakimbizi wakiendesha msako. Kwa takriban saa moja walifanya upekuzi kwenye eneo hilo linalosadikiwa aliwahi kuishi. Kiasi ya polisi 100, pamoja na vitengo maalumu wamehusika kwenye operesheni hiyo katika mji wa Emmerich, uliopo Jimbo la North Rhine Westphalia. Hawakutoa matokeo ya upekuzi huo

Raia waandamana kulaani shambulizi hilo la Berlin.

Kituo cha redio cha RBB kimesema, mtuhumiwa huyo aliacha pochi yake na simu ya mkononi wakati alipokimbia eneo la shambulizi. Waziri wa mambo ya ndani wa Jimbo la North Rhine Westphalia Ralf Jaeger amesema Amri anasadikika kuwa na mawasiliano na mtandao wa mhubiri Abu Walaa anayetajwa kama kiongozi wa misimamo mikali aliyekamatwa hivi karibuni katika mji uliopo Magharibi mwa Ujerumani wa Hildesheim.

Baadhi ya raia wa Berlin wamendamana leo hii,kulaani shambulizi hili huku baadhi wakipinga sera za wakimbizi na wengine wakiunga mkono.

Waziri wa masuala ya usalama Ursulavon der Leyen, aliyetembelea vikosi vya Ujerumani vilivyoko mji wa Mazar-i-Shariff nchini Iraq amesema hawatalegea katika kukabiliana na ugaidi. Georg Pazderski, mwanachama mwandamizi wa chama cha AfD kinachopinga sera za wakimbizi amesema mamlaka zinatakiwa kuwa na msimamo katika kuwarejesha waomba hifadhi waliokataliwa.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amerejelea kiapo chake cha kukabiliana na makundi ya misimamo mikali kwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kuzuia kwa muda wahamiaji wa Kiislamu kuingia Marekani. Alipojibu swali kuhusiana na shambulizi la Berlin, alisema na hapa namnukuu, "Mnajua mipango yangu yote. Nimekuwa nikithibitika kuwa niko sawa. asilimia 100 sawa."  

Kansela wa Ujerumani Angela Merker na waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere jioni hii wamezungumzia shambulizi hilo baada ya kupewa ripoti ya polisi inayohusisha uchunguzi wake.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef