1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ujerumani wachunguza kisa cha lori lililoibiwa

Bruce Amani
8 Oktoba 2019

Polisi Ujerumani inamshikilia raia wa Syria kwa tuhuma za kuiba lori alilolitumia kuyagonga magari yaliyokuwa yamesimama kwenye taa za barabarani katika mji wa Limburg ulioko magharibi mwa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3Qtx6
Deutschland Limburg Lastwagen rammt Fahrzeuge
Picha: picture-alliance/dpa/S. Ditschner

Vyombo vya habari vya Ujerumani viliwanukuu maafisa wa usalama wakisema tukio hilo lililotokea jana jioni linachukuliwa kama ni la kigaidi. Mwendesha mashitaka Ralf Badle amekataa kuzungumzia hilo, lakini akisema linachukuliwa kama jaribio la mauaji. Amesema polisi ilifanya msako kwenye makazi yanayohusishwa na mtuhumiwa na kukamata simu za mkononi na vifaa vya kuhifadhia data na kuongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea. 

Kijana huyo wa miaka 32 alitarajiwa kufikishwa mbele ya jaji ambaye ataamua iwapo kuna haja ya kutoa waranti rasmi wa kukamatwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani – DPA, ni kuwa aliwasili Ujerumani kutokea nchi aliyolaziliwa Syria mwaka wa 2015 na akaishi katika eneo la Offenbach karibu na Frankfurt. Alipewa ulinzi mwaka uliopita – hadhi wanayopewa wale ambao hawatimizi viwango vya kuwa wakimbizi, lakini wako hatarini kama watarejea katika nchi zao walizotoka.

Karte Limburg Hessen EN

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijawa wazi.

Shirika la habari la Umma ZDF, likitaja duru za kiusalama ambazo hazikutajwa, limesema mapema leo kuwa maafisa wanaamini tukio hilo linahusishwa na itikadi kali. Alipoulizwa kama kuwa uwezekano lilikuwa shambulizi la kigaidi, waziri Seehofer aliwaambia wanahabari kabla ya mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg kuwa kwa wakati huu kitendo hicho bado kinachunguzwa.

Ofisi ya mwendesha mashitaka ambayo huzishughulikia kesi za ugaidi nchini Ujerumani, imesema kuwa kwa sasa, haina mamlaka kuhusiana na kesi hiyo, kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha kwamba lilikuwa shambulizi la kigaidi.

Tukio hilo limetokea karibu miaka mitatu baada ya muomba hifadhi wa Kitunisia aliyenyimwa kibali kuwauwa watu 12 kwa kuwagonga na lori katika soko la Krismasi mjini Berlin.