1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Uingereza yawatahadharisha wagombea

Lilian Mtono
15 Novemba 2019

Polisi nchini Uingereza imezindua mbinu mpya za kuwalinda wanasiasa wanaopiga kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Disemba 12, katika wakati ambapo hali ya siasa nchini humo ikitokota na kuwataka kujihadhari.

https://p.dw.com/p/3T7ub
Großbritannien London | Wahl neuer Speaker | Edward Leigh, Kandidat
Picha: Imago Images/ZUMA Press

Viti 650 vya bunge la Uingereza vinawaniwa kwenye uchaguzi huo, na tayari wagombea zaidi ya 70 wamekwishajitoa kwenye kinyang'anyiro hicho na hawatagombea kwa awamu nyingine.

Mkuu wa baraza la kitaifa la wakuu wa polisi nchini humo amesema Ijumaa hii kwamba, jeshi hilo linawataka wagombea kutofanya kampeni peke yao pale inapowezekana, lakini pia kuwasiliana na polisi wa eneo wanapotarajia kwenda mapema kabla ya kufanya kampeni zao.

Jeshi hilo pia linawashauri wagombea kuhakikisha iwapo mambo waliyoyatuma mitandaoni hayaweki wazi "taarifa nyeti za kibinafsi" ambazo zinaweza kuwasaidia wale wenye nia ovu dhidi yao.

UK Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza, Bpris Johnson anatabiriwa kushinda uchaguzi huo kupitia chunguzi za maoniPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Augstein

Mwenyekiti huyo Martin Hewitt amesema ofisi zote za polisi zitatoa taarifa kuhusu usalama kwa wagombea na patakuwepo afisa mwandamizi atakayekuwa akihusika na kusimamia masuala hayo ya kiusalama.

"Hatutawawekea wagombea ukomo wa kampeni lakini tunachukua hatua za mapema na kutoa ushauri unaofaa" alisema. Ushauri huo utatawanywa kwa wagombea wote kama sehemu ya kufurushi cha taarifa za kiusalama zilizoandaliwa na polisi, tume ya uchaguzi na waendesha mashitaka.

Wanasiasa wanaozungumzia kuchelewa kwa mchakato wa Brexitkutoka pande zote wamekuwa wakikabiliwa na vitisho na hata kutishiwa kuuawa, vilivyotolewa moja kwa moja ama kupitia mitandaoni. Miongoni mwao ni wale ambao hawatagombea awamu nyingine kwenye uchaguzi huo.

Lakini pia kumekuwepo na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu usalama binafsi kwa wanasiasa wa Uingereza tangu mbunge wa chama cha Labour Jo Cox alipouawa kwa kuchomwa kisu wakati wa kampeni ya kura ya maoni ya Brexit mnamo mwaka 2016.

Wagombea kadhaa tayari wameripoti kuongezeka kwa vitisho kupitia mitandaoni na kuongezeka kwa visa vya watu wanaoingilia hotuba za wagombea kwa kuwatolea maneno machafu katika siku za mwanzo za kampeni.

UK Wahlkampf Labour Partei
Baadhi ya wafuasi wa chama cha Labour wakiwa kwenye kampeniPicha: picture-alliance/ZUMA WIre/London News Pictures/R. Pinney

Uingereza inafanya uchaguzi mkuu Disemba 12, miaka miwili mapema kwa sababu waziri mkuu Boris Johnson kutoka chama cha Conservative anataka kupata wingi wa viti bungeni, ili kurahisisha mchakato wa kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya ifikapo tarehe ya mwisho ya Brexit Januari 31, 2020.

Kampeni za sasa pia zinaangazia masuala kuhusu ubaguzi wa rangi na hususan msimamo wa chama cha upinzani cha Labour, kuhusu kupambana na chuki dhidi ya Uyahudi. Waandishi maarufu kabisa nchini humo pamoja na wasanii 24 ikiwa ni pamoja na mwandishi John LeCarre na mwigizaji Simon Callow wamesema Ijumaa hii kwamba hawatakipigia kura chama hicho kutokana na kushindwa kwake kukabiliana na chuki dhidi ya Wayahudi.

Aidha, kwenye barua yao wamesema wasiwasi huo unazidi madai kwamba kukiunga mkono chama hicho cha Labour ndio njia pekee ya kukizuia chama cha Conservative cha waziri mkuu Johnson kuiondoa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya kwa makubaliano ama bila ya makubaliano.