1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi kuchukuliwa hatua kuhusu ajali ya barabarani Kenya

Shisia Wasilwa11 Oktoba 2018

Mkuu wa polisi nchini Kenya asema polisi waliozembea kazini wakati ajali ya basi ilitokea na watu 56 kuuawa, watachukuliwa hatua

https://p.dw.com/p/36NO2
Kenia Busunglück
Picha: Getty Images/AFP/B. Ongoro

Polisi waliozembea kazini wakati ilipotokea ajali iliyosababisha vifo vya watu 56 siku ya Jumatano nchini Kenya watachukuliwa hatua za kisheria. Inspekta mkuu wa Polisi Jenerali Joseph Boinett amesema kuwa ni wajibu wa makamanda wa majimbo kuhakikisha kuwa sheria za barabarani zinazingatiwa na madereva katika maeneo yao huku mmiliki wa basi hilo akifikishwa mahakamani. Imebainika kuwa basi hilo lililokuwa likitoka Nairobi kuelekea magharibi mwa Kenya lilikuwa na idadi zaidi ya abiria kinyume cha sheria.

Wakenya wangali wanaomboleza vifo vya watu 56 huku wengine 16 wakiendelea kutibiwa baada ya ajali mbaya kutokea  siku ya Jumatano katika jimbo la Kericho. Ajali hiyo iliyotikisa taifa iliwaleta pamoja maafisa wakuu serikalini kujadili jinsi ya kuzuia matukio kama hayo siku za usoni.

Akizungumza  na waandishi wa habari baada ya mkutano huo Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinett amebainisha kuwa idara ya polisi ni imara wala hakuna matatizo ya majukumu. "Kutekeleza sheria za barabarani ni jukumu la Kamanda wa jimbo na makamanda wake, na wakuu wa vituo vya polisi, kwa hivyo kuhusu ajali ya jana, kamanda mkuu wa jimbo la Kericho anawajibika.”

Watu 56 waliuawa kwenye ajali hii iliyotokea eneo la Kericho tarehe 10.10 2018
Watu 56 waliuawa kwenye ajali hii iliyotokea eneo la Kericho tarehe 10.10 2018Picha: Getty Images/AFP/B. Ongoro

Onyo lake linajiri huku, kukiwa na historia mbaya ya kuwatia nguvuni watu wanaostahili kuwajibika ajali zinapotokea. Huenda yakawa ni maneno matupu kama yale ambayo hutolewa ajali zinapotokea kisha yakasahaulika. Maafisa wa trafiki huwa barabarani kuwachukulia sheria madereva wanaokiuka sheria za barabarani, hivyo yaelekea kuwa basi hilo lilipita kwenye vizuizi vyote vya maafisa wa polisi kutoka Nairobi hadi kwenye jimbo la Kericho kabla ya kuhusika kwenye ajali.

Boinnet amesema watashirikiana na Bodi ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani. Kamanda wa jimbo la Kericho James Mugera amesema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na kuharibika breki kisha basi hilo likabingiria mara kadhaa. Kwa upande wake mkurugenzi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani Francis Meja amefichua kuwa zaidi ya mabasi laki moja hayajazingatia viwango vinavyohitajika. Viwango hivyo vilianza kutekelezwa tarehe 22 mwezi Mei mwaka 2017. "Nina uhakika, idadi ya vifo mnavyoona ingepungua iwapo basi hilo lingekuwa limezingatia muundo wa viwango vinayohitajika.”

Sehemu ya juu ya basi iling'oka yote baada ya dereva kukosa kulidhibiti. Meja amesema kuwa wataanza kuchunguza iwapo mabasi ya uchukuzi wa abiria yamezingatia agizo lao. Mmiliki wa basi hilo amefikishwa mahakamani na atashtakiwa kwa kosa la mauji bila ya kukusudia. Dereva wa basi hilo mwenye umri wa miaka 72 pamoja na utingo wake hawajulikani waliko hadi kufikia sasa. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba watu 62 pekee wala halikuwa na leseni ya kusafiri usiku.