1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya Poland na Umoja wa Ulaya wachacha

Saumu Mwasimba
25 Oktoba 2021

Waziri mkuu wa Poland adai Umoja wa Ulaya wataka kuanzisha vita ya tatu ya dunia na iko tayari kupambana kutetea haki zake

https://p.dw.com/p/42AEE
Deutschland Bundeskanzlerin Merkel in Warschau
Picha: Czarek Sokolowski/AP Photo/picture alliance

Wakati mvutano ukiongezeka kati ya Poland na viongozi wa Umoja wa  Ulaya kuhusu mageuzi katika mfumo wa mahakama nchini Poland,waziri mkuu wa nchi hiyo Mateusz Morawiecki ametoa onyo kali kwa Umoja wa Ulaya kwamba usithubutu kuzuia fedha ilizoahidi kuzitoa kuisaidia nchi yake katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Kiongozi huyo wa Poland amesema kitakachotokea ikiwa halmashauri ya Umoja wa Ulaya itaanzisha kile alichokiita vita vya tatu vya  dunia ni kwamba watatetea haki zao kwa silaha ya aina yoyote watakayokuwa nayo.

Onyo la waziri mkuu huyo wa Poland limetokana na mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Financial Times alipoulizwa ikiwa Poland inaweza kutumia kura yake ya turufu katika masuala kama makubaliano ya kihistoria ya mazingira.

Kilichopo nyuma ya mvutano huu kati ya Poland na Umoja wa Ulaya kimsingi ni uamuzi uliotolewa na mahakama ya katiba ya nchi ya mageuzi ya kimahakama  ambayo kwa sehemu zinakwenda kinyume  na sheria za Umoja wa Ulaya.

Uamuzi huo wa Poland unaangaliwa  na halmashauri ya Umoja wa Ulaya kama tatizo kubwa na nchi nyingine nyingi kwasababu unaweza kuwapa wahafidhina wenye msimamo mkali wa kizalendo wanaoiongoza serikali ya Poland sababu ya kupuuza  maamuzi yatakayokuwa yakitolewa na mahakama ya haki ya Umoja wa Ulaya ECJ ambayo hayawapendezei.

Polen | Urteil Verfassungsgericht | Demonstration in Warschau
Picha: Wojtek Radwanski/AFP/Getty Images

Poland imekuwa ikikosolewa kwa miaka kutokana na mageuzi yake ya mfumo wa mahakama .Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von Der Leyen ameshasema kwamba  atazuia   kupelekwa Poland msaada wa mabilioni ya yuro za kusaidia katika janga la Corona mpaka pale nchi hiyo itakaporekebisha baadhi ya mageuzi yake ya kimahakama.

Lakini Morawiecki anasema Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inakiuka sheria ya Umoja huo kwa aidha kuidhinisha au kuinyima Poland msaada  na nchi hiyo iko tayaro kusubiri kupokea fedha hizo.

Waziri mkuu huyo wa Poland anasema kwamba hawapaswi kuzungumza na Umoja wa Ulaya wakiwa wameshikiana bunduki kichwani. Msemaji wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya leo Jumatatu alinukuliwa akisema kwamba Umoja huo hauwezi kutoa tamko kuhusu taarifa iliyotokana na mahojiano.