Pigo kwa makubaliano ya usalama Afganistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Pigo kwa makubaliano ya usalama Afganistan

Makubaliano ya usalama kati ya Afghanistan na Marekani yazidi kupata pigo kabla ya kusainiwa baada ya kuuwawa kwa mvulana wa miaka minne na uamuzi wa serikali kuwaachilia wafungwa wengi wa Taliban.

Wafungwa katika gereza la Bagram Afghanistan.

Wafungwa katika gereza la Bagram Afghanistan.

Mpatanishi wa Marekani katika mazungumzo ya kufanikisha makubaliano ya usalama kati ya nchi hiyo na Afghanistan ameonya kwamba ni jambo lisiloyumkinika kwa Rais Hamid Kazai kusaini makubaliano hayo kwa wakati unaotakiwa,onyo lake hilo linakuja wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukizidi kuathirika baada ya serikali ya Afghanistan kutangaza hapo jana kwamba itawachia huru wafungwa wengi wa Taliban ambao Marekani inawaona kuwa ni hatari na wanaweza kurudi tena kwenye mapambano.

Balozi James Cunningham wa Marekani ametowa onyo hilo katika tathmini yake kwenye waraka wa siri hivi karibuni baada ya serikali ya Rais Barack Obama kuendelea kuongeza muda mara kadhaa wa kufikiwa kwa makubaliano hayo ambayo awali yalikuwa yasainiwe katika kipindi cha majira ya mapukutiko mwaka jana.

Wakati unayoyoma

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amesema wiki hii makubaliano hayo lazima yasainiwe katika kipindi cha wiki kadhaa na sio miezi na kwamba wakati unayoyoma.

Lakini Cunningham amesema hatarajii Karzai atakubali kusaini makubaliano hayo kabla ya ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi wa Aprili.

Vikosi vya Marekani leo hii vimemuuwa kumpiga risasi kwa bahati mbaya mvulana wa miaka minne katika mkoa wa kusini wenye vurugu wa Helmand. Imeelezwa kuwa kutokana na hali ya hewa kuwa ya mavumbi wanajeshi wa Marekani walimdhania mtoto huo kuwa ni adui na hiyo kumpiga risasi.

Uhusiano wa Afghanistan na Marekani umeathirika kutokana na Rais Hamid Karzai kugoma kusaini makubaliano ya usalama baina ya nchi hizo mbili ambayo yangeliruhusu uwepo wa majeshi ya Marekani nchini humo baada ya kuondolewa kwa takriban vikosi vyote vya kigeni nchini humo mwaka huu.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.

Karzai anataka Marekani kukomesha operesheni zake za kijeshi inazozifanya bila ya ushauriano na serikali ya Afghanistan katika ardhi ya nchi hiyo miongoni mwa mambo mengine kwa sababu zinasababisha maafa kwa raia ambayo yanaweza kuepukwa.

Wafungwa wa Taliban kuachiliwa

Katika kile kinachoonekana kuwa kitazidi kuudhofisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hapo jana serikali ya Afghanistan imesema itawaachilia wafungwa wengi wa Afghanistan kutoka kwenye magereza kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha dhidi yao licha ya pingamizi za Marekani kwamba watu hao wanaweza kurudi tena kwenye mapambano wakati vikosi vya Jumuiya ya Kujihami vya NATO vikiondoka nchini humo.

Msemaji wa Rais Karzai amesema serikali ina ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka wafungwa 16 tu kati ya 88 ambao Marekani inawaona kuwa ni hatari kwa usalama na kwamba inapanga kuwaachilia huru wale waliobakia.

Wapiganaji wa Taliban wakiwa chini ya ulinzi wa wanajeshi wa Afghanistan.

Wapiganaji wa Taliban wakiwa chini ya ulinzi wa wanajeshi wa Afghanistan.

Marekani inapinga vikali kuachiliwa kwa wafungwa hao kwa sababu inasema wamehusika katika kuwajeruhi au kuwauwa wanajeshi wa Marekani na wale wa muungano nchini humo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amesema Marekani inawaona wafungwa 72 miongoni mwa hao wanaoshikiliwa kuwa ni hatari.

Amesema wakati utasema iwapo kuachiliwa kwa wafungwa hao kutaathiri kusainiwa kwa makubaliano ya usalama kati ya nchi hizo mbili ambayo ni kwa ajili ya maslahi ya nchi hiyo ya Afghanistan.

Seneta John McCain (kushoto) na seneta Lindsey Graham.(kulia).

Seneta John McCain (kushoto) na seneta Lindsey Graham.(kulia).

Maseneta wa Marekani waliokuwa wakiitembelea Afganistan wiki iliopita wamesema kuachiliwa kwa wafungwa hao kutaathiri uhusiano wa nchi hizo kuwa katika hali isioweza kurekebishwa lakini hawakusema kwamba kutasababisha kuondolewa kikamilifu kwa wanajeshi wa Marekani.

Hapo jana Seneta John McCain na mwenzake Lindsey Graham wamesema wamemweleza wazi Karzai mjini Kabul wiki iliopita juu ya kupinga kwao kuachiliwa kwa wafungwa hao na kwamba kuna hatua zitakazochukuliwa kukabiliana na uamuzi wa serikali ya Afghanistan.

Katika tukio jengine tafauti wanajeshi wawili wa Marekani na raia mmoja wameuwawa katika kile kilichoelezwa kuwa ni ajali ya ndege mashariki ya Afghanistan leo hii.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com