1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Coutinho ni moto wa kuotea mbali

16 Desemba 2019

Philipe Coutinho ndiye aliyekuwa nyota katika mechi za Bundesliga mwishoni mwa wiki kwa kuwa alifunga magoli matatu katika mechi dhidi ya Werder Bremen Bayern Munich wakipata ushindi wa sita kwa moja huko Allianz Arena.

https://p.dw.com/p/3UuOG
Bundesliga Fußball FC Bayern München | Fussballspieler | Philippe Coutinho
Picha: Reuters/M. Dalder

Robert Lewandowski aliongeza idadi ya mabao yake kwenye Bundesliga msimu huu kwa kufunga mawili kisha Thomas Müller akapata bao moja.

Fußball: Bundesliga, FC Bayern München - Werder Bremen
Coutinho akifunga goli lake la tatu dhidi ya BremenPicha: picture-alliance/dpa/M. Balk

Katika mechi zengine RB Leipzig walipata ushindi wa tatu bila walipokuwa ugenini wakicheza na Fortuna Düsseldorf na ushindi huo uliwapelekea kukwea hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani baada ya waliokuwa vinara Borussia Mönchengladbach kutetereka walipofungwa mbili moja na Wolfsburg.

Borussia Dortmund walivuna ushindi mnono wa nne bila licha ya kuwa ugenini wakivaana na Mainz ambapo nahodha Marco Reus, Jadon Sancho, Thorgan Hazard na Nico Schulz ndio waliotikisa wavu katika mtanange huo.

Bundesliga - 1.FSV Mainz 05 - Borussia Dortmund
Jadon Sancho akiwafungia Dortmund dhidi ya MainzPicha: Getty Images/AFP/D. Roland

Tukiangazia msimamo wa Bundesliga kwa sasa ni kwamba Leipzig wako kileleni wakiwa na pointi thelathini na tatu Borussia Moenchengladbach wanawafuata kwa karibu pointi zao zikiwa thelathini na moja halafu Borussia Dortmund ni wa tatu wakiwa na pointi ishirini na tisa.

Schalke ni wa nne na alama ishirini na nane kisha mabingwa Bayern Munich wana pointi ishirini na saba katika nafasi ya tano. Chini ya jedwali kuna Fortuna Düsseldorf katika nafasi ya kumi na sita kumi na saba wako majirani wao FC Köln kisha mkia ni wa SC Paderborn.

Wafungaji bora wanaongozwa na Mpoland Robert Lewandowski mwenye mabao kumi na nane halafu Timo Werner wa Rb Leipzig ana mabao kumi na sita kisha Rouwen Hennings wa Düsseldorf ana mabao kumi katika nafasi ya tatu akifuatiwa kwa karibu na Marco Reus wa Dortmund mwenye mabao tisa.