1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

Pasi ya chanjo ya EU: Changamoto ya kimaadili na kisheria?

Saumu Mwasimba
4 Machi 2021

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inataka kuanzisha hati maalum ya chanjo ya kidijitali kurahisisha ussfiri kwa watu waliopata chanjo ya Covid-19 ndani na nje. Je, hati hii ni changamoto nyingine ya kimaadili na kisheria?

https://p.dw.com/p/3qCwT
Symbolbild Digitaler Covid-19-Impfausweis
Picha: ActionPictures/imago images

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen siku ya Jumatatu aliandika ujumbe katika ukurasa wa Twitta uliosema kwamba hati ya kusafiri ya chanjo ya Covid-19, au kile kinachoitwa Digital Green Pass ni hati itakayorahisisha maisha ya watu wa ulaya, ikilenga hasa kuwawezesha hatua kwa hatua kusafiri salama katika nchi za Umoja wa Ulaya au nje ya umoja huo kwa ajili ya shughuli za kikazi au utalii.

Nchi za kusini mwa Ulaya kama Ugiriki na Cyprus ambazo uchumi wake unategemea zaidi shughuli za utalii zimehusika sana katika kutia msukumo wa kuanzishwa hati hiyo ya chanjo wakati zikijaribu kufufua sekta hiyo ya utalii katika nchi zao ambayo imepata pigo kubwa sana.

Lakini mpango huu unatarajiwa kuchukua muda wa miezi mitatu kuweka mifumo ya uhakika katika suala la kiufundi na kimiundombinu ya usafiri. Na hapo ndipo linapokuja tatizo.

Melinda Mills, mkurugenzi wa kituo cha masuala ya sayansi kuhusu idadi ya watu katika chuo cha Oxford ameiambia DW kwa njia ya barua pepe kwamba kabla ya kuanzishwa pasi hiyo watu wengi watapaswa kupata chanjo na watu wengi watahitaji kuwa nazo.

Symbolfoto Digitaler Impfpass, Impfbestaetigung.
Pasi ya chanjo inalenga kuwarahisishia rais kusafiri ndani na nje ya Umoja wa Ulaya kwa uhuru zaidi.Picha: Frank Hoermann/SVEN SIMON/picture alliance

Kwa Ulaya, mipango iliyopo sasa inaonesha kwamba kiasi asilimia 70 ya watu wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya watachanjwa kufikia mwishoni mwa msimu wa joto mwaka huu. Lakini kufikia sasa ni asilimia 6 tu ya watu katika nchi hizo waliochanjwa.

Kwa mujibu wa halmashauri ya umoja huo, kibali hicho au hati hiyo ya kidijitali ya chanjo itakwenda mbali zaidi ya kuorodhesha tu aina ya chanjo uliyopata na historia yako ya kiafya, lakini pia itaangalia taarifa nyingine ili kuepusha ubaguzi wa raia.

Soma pia:EU: Yapendekeza pasi maalum ya chanjo ya virusi vya corona

Kwa mfano "suala la majibu ya kimatibabu pamoja na taarifa za kutibiwa kwa mwenye hati hiyo," alibainisha msemaji wa halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya Christian Wigand siku ya Jumatatu.

Masuala mazito kuhusu maadili na sheria

Hata hivyo suala kubwa linalotarajiwa kuzusha mjadala ni kuhusu viwango vya maadili na suala la faragha. Suala kubwa hapa la kimaadili linaloleta wasiwasi ni kwanza kuamua ni nani anayepaswa kuwekwa kando katika mpango huu ikiwa utaanzishwa.

Kadhalika Mills anasema kuna baadhi ya makundi ya watu ambayo hayawezi kuchanjwa kutokana na sababu za kiafya mfano wale wenye matatizo ya mzio au wajawazito.

Na isitoshe katika baadhi ya nchi jamii fulani za walio wachache zinapingana na utaratibu wa chanjo, hali ambayo ni dhahiri itamaanisha kwamba jamii hizi zinaweza kutengwa katika mpango huu.

Belgien EU Parlament Covid-19 Impfungen Ursula von der Leyen
Rais wa Halashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.Picha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Ripoti iliyotayarishwa kwa ushirikiano na Mills na kuchapishwa na taasisi inayoshughulikia masuala ya dharura ya kisayansi iliyopewa jukumu kushughulikia suala la Covid-19, imebaini masuala kadhaa ambayo yanahitaji kuangaliwa kabla ya mpango huo wa hati ya chanjo haujaanzishwa.

Na mmoja wa waandishi wengine wa ripoti hiyo, Chris Dye ambaye ni Profesa wa magonjwa ya miripuko katika idara ya magonjwa ya wanyama, katika chuo cha Oxford anasema licha ya hatua kadhaa kupigwa katika masuala ya maadili, faragha na kiufundi, bado kuna mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi.

Lakini pia ikumbukwe, moja ya majukumu makubwa ya mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu (ECHR)ni kulinda taarifa za kiafya za raia wa Ulaya lakini pia kuzuia ubaguzi linapokuja suala la chanjo kwa kuzingatia masuala ya umri, kabila au jinsia.