1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Vikosi huenda vikapelekwa Darfur mapema mwakani

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBoJ

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa,Hervé Morin amesema, kikosi kipya cha kimataifa huenda kikapelekwa Darfur mapema mwakani,katika bidii ya kutaka kukomesha mapigano katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.Waziri Morin alikuwa akizungumza mwishoni mwa mkutano uliofanywa mjini Paris,kwa azma ya kuchangamsha utaratibu wa amani katika Darfur.Amesema,vikosi vya Ufaransa huenda vikawa sehemu kubwa ya wanajeshi 20,000 wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika watakaopelekwa Darfur.

Wakati huo huo waziri wa nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema,mkutano huo wa Paris unaunga mkono juhudi za kisiasa za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.Akaongezea kuwa Darfur,tayari wapo wanajeshi.Lakini wanajeshi hao hawakuandaliwa vizuri na hawalipwi.Maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuongeza idadi ya wanajeshi wasiolipwa,alieleza waziri wa nje wa Ufarsansa Kouchner.

Mapema mwezi huu Rais Omar al-Bashir alikubali kuruhusu vikosi vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kupelekwa Darfur.Hadi watu 200,000 wameuawa na wengine milioni 2.5 wamelazimishwa kuondoka makwao,tangu kuanza kwa mgogoro wa Darfur miaka minne iliyopita.