1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Sarkozy ataka ratiba ya kuondoka majeshi Irak

27 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBVN

Rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa leo ametaka kuwepo ratiba ya kuwaondoa wanajeshi wa kigeni walio nchini Irak huku akiendeleza ushawishi wa Ufaransa katika maswala mengine tete duniani.

Akitoa hotuba yake ya kwanza tangu alipoingia madarakani, rais Sarkozy amekumbusha kwamba Ufaransa ilipinga vita dhidi ya Irak mnamo mwaka wa 2003, lakini akasema sasa iko tayari kuisadia jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhisho la kisiasa.

Rais Sarkozy pia ametaka Ulaya ijimaarishe katika sera zake za kigeni.

´Mimi ni miongoni mwa wanaoamini kwamba hakuna Ufaransa imara bila Ulaya na hakuna Ulaya imara bila Ufaransa. Mimi ni miongoni mwa wanaoamini urafiki kati ya Marekani na Ufaransa leo ni muhimu kama ulivyokuwa miongo miwili iliyopita.´

Rais Sarkozy amehutubia muda mfupi baada ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner, kulazimika kuomba radhi kwa kupendekeza waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki ajiuzulu wakati wa ziara yake mjini Baghdad kati ya tarehe 19 na 21 mwezi huu.

Nuri al Maliki jana aliitaka serikali ya Ufaransa iombe radhi rasmi baada ya waziri Kouchner kuashiria katika toleo la jarida la Newsweek la Marekani kwamba waziri mkuu huyo wa kishia analazimika kuondoka madarakani.