Papa Francis ziarani Korea Kusini | Masuala ya Jamii | DW | 14.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Papa Francis ziarani Korea Kusini

Papa Francis amewasili Korea ya Kusini kwa ziara ya siku tano, ikiwa ni ya kwanza baada ya robo karne katika nchi inayotambuliwa kama alama ya mafanikio ya kanisa katika eneo la mashariki ya mbali.

Papa Francis (kushoto) akisindikizwa na mwenyeji wake, Rais Park Geun-hye, kukagua gwaride la heshima kwenye Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Seongnam, tarehe 14 Agosti 2014.

Papa Francis (kushoto) akisindikizwa na mwenyeji wake, Rais Park Geun-hye, kukagua gwaride la heshima kwenye Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Seongnam, tarehe 14 Agosti 2014.

Papa alipokelewa kwenye uwanja wa jeshi kusini mwa mji mkuu, Seoul, na Rais Park Geun-hye, raia wawili wa Korea ya Kaskazini waumini wa Kanisa lake na jamaa wa wahanga wa ajali ya meli ya Sewol iliyozama mwezi Aprili na kuua kiasi cha abiria 300, wengi wao wanafunzi wa skuli.

Lengo kuu la ziara hiyo ya Papa Francis ni kuhudhuria Siku ya Vijana wa Asia, hafla inayotazamiwa kuwakusanya pamoja washiriki 6,000, robo yao kutoka nje ya nchi hiyo. Hata hivyo, msemaji wa ziara hiyo ya Papa, Heo Young-yeop, amesema wamesikitishwa na kitendo cha kuzuiliwa zaidi ya nusu ya washiriki 100 wa kongamano hilo kutoka China kufika Korea ya Kusini.

"Baadhi ya vijana wa Kichina ambao walikuwa wamepanga kuja kwenye hafla hii hawakuweza kuja kutokana na hali mbaya nchini China. Kamati inasikitika sana kwa hilo," Heo aliwaambia waandishi wa habari.

Ingawa msemaji huyo wa ziara ya Papa alikataa kueleza undani wa mkasa huo, akisema anahofia usalama wao, muandaaji mwengine alisema baadhi ya waalikwa hao wamekamatwa na mamlaka nchini China.

China, Vatican hazina mahusiano mazuri

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, akipokelewa na watoto wa Korea ya Kusini alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Seongnam, tarehe 14 Agosti 2014.

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, akipokelewa na watoto wa Korea ya Kusini alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Seongnam, tarehe 14 Agosti 2014.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China haikutoa kauli yoyote juu ya suala hilo wala juu ya ujumbe wa Papa Francis kwa nchi hiyo. Akiwa angani kuelekea Seoul, Papa Francis alituma ujumbe wa nia njema kwa China wakati ndege yake ikipita juu ya anga la nchi ambayo haiwaruhusu raia wake walio waumini wa Kanisa Katoliki kutambua mamlaka ya Papa huyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa papa kuruhusiwa kuruka kupitia anga la China katika ziara zake za Asia. Mtangulizi wake, John Paul II, alikuwa akiepuka kutumia anga la China kwa sababu ya mahusiano mabaya kati ya Beijing na Vatican. Tangu Chama cha Kikomunisti kuchukua madaraka hapo mwaka 1949, pande hizo mbili hazina mahusiano rasmi.

Kanisa Katoliki nchini China limegawika kwenye jamii mbili: kanisa "rasmi" ambalo linawajibika kwa chama na kanisa la chini kwa chini ambalo linamtii papa wa Vatican tu.

Wakati Papa Francis akiwasili Korea ya Kusini, taarifa zinasema utawala hasimu wa Korea ya Kaskazini umefanya majaribio ya silaha zake kwenye pwani ya nchi hiyo. Kama ilivyo China, Korea ya Kaskazini nayo haikubaliani na mamlaka ya Kanisa Katoliki kwa raia wake.

Hii ni ziara hii ya tatu kimataifa kwa Papa Francis tangu achaguliwe Machi mwaka jana na hailengi tu kwenye kuwafikia waumini milioni tano wa kanisa lake nchini Korea ya Kusini, bali pia waumini wote wa Asia Mashariki, kwani tangu alipochaguliwa aliahidi kwamba angeliweka msisitizo maalum kwa bara la Asia.

Mwandishi: Klaus Dahman/Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Char

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com