Papa Francis kuanza ziara Marekani leo | Masuala ya Jamii | DW | 22.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Papa Francis kuanza ziara Marekani leo

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis leo anaondoka Cuba ambako amepokelewa kwa shangwe, kuelekea Marekani ambako ingawa pia anapendwa, anakosolewa na wahafidhina kwa msimamo wake kuhusu maskini na mazingira.

Papa Francis Leo anafanya ziara yake ya kwanza nchini Marekani

Papa Francis Leo anafanya ziara yake ya kwanza nchini Marekani

Papa Francis anamaliza ziara yake ya Cuba leo Jumanne, kwa kuongoza misa katika madhabahu maarufu zaidi nchini humo, na atafanya mazungumzo na familia kabla ya kupanda ndege kuelekea katika mji mkuu wa Marekani, Washington.

Mazungumzo na familia pamoja na ziara yake Marekani ni shughuli mbili zinazoeleza sababu kubwa ya kuizulu Cuba, ambayo ni kuhimiza maridhiano ndani ya familia, na pia baina ya Cuba na Marekani. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani alitoa mchango mkubwa katika kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili hivi karibuni.

Nchini Cuba ratiba ya kazi ya Papa Francis ilikuwa na mambo chungu nzima; ameongoza ibada katika miji miwili kati ya mitatu aliyoitembelea, ameshiriki katika misa za kuwaombea watu, ameshikana mikono na maelfu ya watu, na pia, amefanya mazungumzo na rais wa Cuba Raul Castro, pamoja na mtangulizi wake ambaye pia ni kaka yake, Fidel Castro.

Hafurahiwi na wahafidhina

Nchini Cuba Papa Francis amepokelewa kwa shangwe kubwa

Nchini Cuba Papa Francis amepokelewa kwa shangwe kubwa

Mjini Washington ambako anatarajiwa kuwasili leo, Papa huyo atapokelewa na rais Barack Obama na mke wake, na baadaye ataendelea na orodha ndefu ya shughuli, ikiwepo hotuba kwenye kikao cha pamoja cha bunge la Marekani, Congress na atalihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba asilimia 66 ya wamarekani wanamuunga mkono Papa Francis, lakini pia wapo wanasiasa wasiopendezwa na msimamo wake ambao unaonekena kuegemea upande wa kushoto. Mmoja wa wabunge wa nchi hiyo Paul Gosar ambaye ni mkatoliki, amesema hatahudhuria hotuba ya kiongozi huo wa kanisa, ambaye anamtuhumu kuwa na mtazamo wa kisoshalisti.

''Badilika wewe kwanza, kisha ndipo uwakosoe wengine''

Pia wapo wahafidhina wa kimarekani ambao wangependa kumsikia Papa akipigia debe mabadiliko ya kisiasa nchini Cuba. Kuhusu suala hilo, msemaji wa Papa Francis Padri Federico Lombardi, ameuelezea msimamo wa kiongozi wake.

''Anachomjibu Papa Francis mtu anaemuuliza swali hilo, ni ''badilika kwanza wewe''. Kila mmoja wetu anapaswa kwanza kufikiria anavyoweza kubadilika mwenyewe, kisha ndio atoe ushauri kwa wengine kubadilika''. Amesema Padri Lombardi.

Msimamo Papa Francis kuwatetea masikini, kutaka hatua kali za kuhifadhi mazingira ya dunia, na kukemea mtindo wa sasa wa maisha wa kuabudu pesa, unaonekana kwenda kinyume na kile kinachoaminika kuwa maadili ya Kimarekani.

Papa Francis atalihutubia Bunge la Marekani Alhamis na baadaye Ijumaa atakwenda mjini New York katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com