1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awaombea wahanga wa hujuma za kundi la IS

7 Machi 2021

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis aliye ziarani nchini Iraq leo Jumapili amewaombea wahanga wa madhila ya kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

https://p.dw.com/p/3qK5A
Irak Karakosch | Besuch Papst Franziskus
Picha: Yara Nardi/REUTERS

Ibada hiyo imefanya katika mji wa Mosul uliowahi kuwa moja ya ngome imara ya kundi la IS.

Papa Francis ameitumia siku yake ya tatu katika ziara ya siku nchini Iraq kutuma ujumbe wa mshikamano na jamii ya wakristo wa Iraq ambao idadi yao imeendelea kupungua katika miaka ya karibuni kutokana na vita na unyanyasaji.

Papa alikwenda mji wa kaskazini wa Mosul, uliokuwa chini ya wapiganaji wa kundi la IS kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 akitokea Erbil ambao ni mji mkuu wa jimbo lenye mamlaka ya ndani linalokaliwa na jamii za wakurdi.

"Kwa kuwa Mungu ni Mungu wa amani ni makosa kwetu kuendesha vita kwa jina lake" amesema Papa Francis akiwa kwenye eneo la Hosh al-Bieaa, yanakokutikana makanisa manne yaliyoharibiwa vibaya na mapigano.

"Kwa kuwa Mungu ni Mungu wa upendo, ni makosa kwetu kuwachukia ndugu na jamaa zetu" aliongeza kusema Baba Mtakatifu.

Papa Francis: Ugaidi na mauaji havina usemi wa mwisho 

Akiongoza ibada hiyo Papa Francis amesema anaitumia siku ya Jumapili kuwaombea wahanga wote wa machafuko kwa Mungu mwenyezi.

Irak Mosul | Besuch Papst Franziskus
Picha: Andrew Medichini/AP/picture alliance

Kiongozi huyo pia ameelezea huzuni yake kwa jinsi matendo ya kinyama yanayofanywa kwa kutimia jina la dini yalivyoharibu majengo ya ibada na turathi nyingine nchini Iraq.

Kwenye ziara hiyo mjini Mosul, Baba Mtakatifu pia ameyazuru mabaki ya mji huo na kuomba akiwa kwenye maeneo tofauti.

Papa pia ameutembelea mji mdogo wa Qaraqosh ulio kiasi kilometa 30 mashariki ya Mosul ambao ulikuwa makaazi ya jamii kubwa ya wakristo hadi pale kundi la IS lilipouharibu na kuwalazimisha watu wengi kuukimbia.

"Kukusanyika kwetu hapa leo kunaonesha ugaidi na vifo havikuwa na usemi wa mwisho" amesema Papa Francis akiwaambia wale waliokusanyika kwenye kanisa kuu la Immaculata lililokarabatiwa mjini Qaraqosh.

Ziara ya wito wa amani na kusameheana 

Irak Najaf | Besuch Papst Franziskus | Großajatollah Ali al-Sistani
Papa Francis na kiongozi wa waislamu wa Shia nchini Iraq, Ulamaa Ali al-Sistani.Picha: Ayatollah Sistani's Media Office/AFP

Kwa sehemu kubwa ujumbe wa Papa Francis kwenye zaira nchini Iraq ni kutoa wito wa amani na msamaha hasa kwa jamii za wakristo wanaolengwa na wapiganaji wa itikadi kali.

Inakadiriwa kulikuwa na zaidi ya wakrsito milioni 1 nchini Iraq lakini idadi yao imepungua na kufikia kati ya 250,000 hadi 400,000 baada ya miongo kadhaa ya vita, unyanyasaji wa kidini na hali ngumu ya uchumi.

Vatican inatumai ziara ya Baba Mtakatifu ambayo ni ya kwanza kufanya na kiongozi wa kanisa katoliki itafufua matumaini ya wakristo wa Iraq.

Papa Francis aliwasili Baghdad siku ya Ijumaa kwa ziara ya siku akipuuza kitisho cha usalama pamoja na janga la virusi vya corona.

Katika siku ya pili hapo Jumamosi alikwenda kwenye mji mtakatifu wa Najaf kukutana na kiongozi wa Waislamu wa Shia nchini Iraq Ayatollah Ali al-Sistani.

Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza kwa viongozi hao wa dini mbili tofauti ulinuwia kuonesha umuhimu wa kuishi pamoja licha ya tofauti za imani.