1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa ashindwa kuwaridhisha wahanga wa ubakaji

Saumu Mwasimba
22 Februari 2019

Katika mkutano wa kilele unaoendelea kuhusu kuzuia unyanyasaji wakingono dhidi ya watoto,kiongozi wa kanisa Katoliki ashindwa kuidhinisha hatua iliyopendekezwa na waliopitia ubakaji la kutaka wahusika wafukuzwe kanisani

https://p.dw.com/p/3DqRv
Vatikan Missbrauchs-Gipfel: Papst fordert konkrete Maßnahmen von Bischöfen
Picha: Reuters/Vatican Media

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amejiandaa leo (22.02.2019)  kuendelea kuongoza kikao cha mkutano wa kilele wa Kanisa Katoliki kuhusu kuzuia unyanyasaji wakingono dhidi ya watoto unaotajwa kufanywa na viongozi wa kidini wa kanisa hilo.

Katika siku hii ya pili ya mkutano wa siku nne itashuhudia hotuba zikitolewa,pamoja na kuwepo kipindi cha maswali na majibu sambamba na kuwepo majopo kazi,vipindi vya maombi na kusikilizwa ushuhuda utakaotolewa na wahanga waliobakwa na waumini wa kanisa katoliki. Katika ufunguzi wa mkutano huo hapa jana kiongozi mkuu wa kanisa Papa Francis aliwasilisha mpango wa pointi 21 wa kupambana na vitendo vya unyanyasaji kingono katika kanisa hilo pamoja na kuwahusisha wataalamu wasiokuwa waumini wa dini katika uchunguzi wa ndani wa kanisa hilo.

Vatikan Gipfel zum Thema sexueller Missbrauch in der Kirche
Picha: Reuters TV

Hata hivyo Papa Francis alishindwa kwenye mpango wake kuidhinisha pendekezo muhimu lililotolewa na wahanga waliofanyiwa madhila ya ubakaji la kutaka mapadri wote waliotajwa kuhusika na vitendo hivyo viovu pamona na maaskofu waliouficha uhalifu huo kufukuzwa kabisa kanisani. Sauti mbali mbali za viongozi wa kanisa hilo zilisikika jana zikitowa ujumbe wa hisia kuhusu dhambi hiyo ya ubakaji iliyolichafua kanisa Katoliki duniani. huyu hapa ni kadinali Luis Tangle kutoka Ufilipino.

''Kushindwa kwetu kushughulikia mateso waliyoyapata wahanga,na hata kufikia hatua ya kuwakataa na kuficha kadhia hii ili kuwalinda waliotajwa kuhusika pamoja na taasisi,kumewaumiza watu,na kusababisha vidonda vikubwa katika mahusiano yetu na wale tuliotumwa kuja kuwatumikia''

Vatikan Missbrauchs-Gipfel: Papst fordert konkrete Maßnahmen von Bischöfen
Tim Lennon rais wa mtandao wa walionusurika na ubakaji uliofanywa na mapadriPicha: picture-alliance/dpa/L. Navarra

Wahanga waliobakwa pia walipata nafasi ya kusikika katika kikao cha jana.akiwemo mhanga kutoka Chile aliyewaita walioshiriki mkutano huo kuwa wauwaji wa imani.Alikuwepo pia mwakanamke wa kiafrika aliyezungumza kwa hisia na kusimulia jinsi alivyobakwa kwa miaka 13 vitendo alivyoanza kufanyiwa akiwa na umri wa miaka 15 akiwa chini ya mikono ya padri wake wa kikatoliki.

Zaidi ya miaka 30 baada ya kadhia hii ya ubakaji makanisa kuibuliwa nchini Ireland na Australia,na miaka 20 baada ya kugonga vichwa vya habari nchini Marekani wakihusishwa maaskofu na maafisa wengine wa kanisa Katoliki barani Ulaya,Amerika ya Kusini,bado hadi wakati huu barani Afrika na Asia viongozi wa kidini wa kanisa hilo ama wanakanusha au kukataa kabisa kwamba visa vya ubakaji vipo katika kanisa katoliki kwenye maeneo yao.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga