1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis apeleka ujumbe wa umoja na maridhiano Msumbiji.

Tatu Karema
5 Septemba 2019

Baba mtakatifu Francis ameanza ziara nchini Msumbiji, akitarajiwa kutoa hotuba mbele ya viongozi wa serikali na wa chama cha upinzani, ambao  hivi karibuni walitia saini mkataba wa amani.

https://p.dw.com/p/3P3CE
Mosambik Papst Franziskus und President Filipe Nyusi und seine Frau in Maputo
Picha: Reuters/Y. Nardi

Maelfu ya wakazi wengine wakivalia skati  zilichorwa sura ya baba mtakatifu na maneno ya, ''matumaini, amani na maridhiano'' wamemiminika katika barabara za mji mkuu, Maputo.

Watu hao wameshangilia msafara wa magari wa baba mtakatifu alipokuwa akielekea katika ikulu leo Alhamisi kukutana na rais Felipe Nyusi. Baadaye, baba mtakatifu anatarajiwa kutoa taarifa.

Ziara hii ya Papa Francis inajiri mwezi mmoja baada ya serikali kutia saini mkataba wa kihistoria wa amani na lililokuwa kundi la upinzani la Renamo ambalo sasa ndicho chama kikuu cha upinzani.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji vilivyodumu kwa miaka 16 vilitatiza taifa hilo lililokuwa koloni la Ureno na kusababisha vifo vya takriban watu milioni moja  na kundi hilo la Renamo halijawahi kuweka chini silaha zake kikamilifu.

Francis, Papa wa kwanza kuzuru Msumbiji tangu Papa John Paul wa pili kufanya ziara nchini humo mnamo mwaka 1988, ameanza siku yake leo Alhamisi kwa mkutano wa faragha na rais Filipe Nyusi anayetaka kuwania muhula wa pili ofisini katika uchaguzi uliopangiwa kufanyika tarehe 15 mwezi Oktoba.

Wawili hao walikuwa tayari wamekutana mwaka mmoja uliopita mjini Vatican.

Mbali na kuzungumzia mkataba huo wa amani, Francis anatarajiwa kuzungumzia uharibifu uliosababishwa na vimbunga viwili vilivyofuatana mapema mwaka huu katika taifa hilo maskini zaidi katika eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika.

Baba mtakatifu hatafanya ziara katika mji wa Beira nchini humo uliosombwa na kimbunga cha Idai mwezi Machi na kusababisha vifo vya watu 600 na kuwaacha maelfu bila makazi. Hata baada ya kukamilika kwa muda wa miezi sita baada ya tukio hilo, baadhi ya watu bado hawana makazi na chakula.

Hapo kesho Ijumaa, Papa Francis atawahutubia wananchi katika uwanja wa michezo wa Zimpeto mjini Maputo. Pia atazungumzia suala la itikadi kali Kaskazini mwa Msumbiji ambapo mashambulizi ya vita vya kidini yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 katika muda wa zaidi wa miaka miwili.

Baadaye baba mtakatifu atafanya ziara nchini Madagascar na Mauritius , mataifa ya visiwa yalioko Mashariki ya Pwani ya Afrika.