1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahimiza mshikamano katika vita dhidi ya corona

Bruce Amani
12 Aprili 2020

Mabilioni ya watu kote duniani wamesherehekea Jumapili ya Pasaka wakiwa majumbani mwao huku kiongozi wa kanisa katoliki duniani akitoa wito wa mshikamano katika kupambana na janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3ao61
Vatikan | Papst Franziskus während Ostermesse im Petersdom
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Taswira zisizo za kawaida za makanisa yasio na watu ziliibuka kutokea Italia hadi Pana na Ufilipino, huku viongozi w akidini wakitafuta mbinu za ubunifu za kuwahutubia waumini katika kuadhimisha siku kuu ya pasaka wakiwa majumbani mwao.

Zaidi ya nusu ya ulimwengu -- Zaidi ya watu bilioni nne – wamebakia majumbani mwao kote duniani wakati serikali zikipambana kuzuia kusambaa kwa janga hilo ulimwenguni.

Ulaya ndilo bara lililoathirika pakubwa na leo imeweka rekodi ya kufikisha jumla ya idadi ya vifo 75,000 kwa mujibu wa takwimu za AFP.

Marekani inaendelea kuwa kitovu cha janga hilo, na mpaka sasa imefikisha Zaidi ya vifo 20,000, kati ya karibu watu nusu milioni walioambukizwa.

Papst Franziskus  Messe Ostern Vatikan
Misa ya pasaka imefanyika bila ushiriki wa wauminiPicha: Reuters/G. Mangiapane

Akizungumza katika Kanisa la Mtakatifu Paulo ambalo lilikuwa na watu wachache mno, ujumbe wa Jumapili ya Pasaka wa Papa Francis ulilenga kwa kiasi kikubwa katika janga hilo, akiwaombea wagonjwa na kuyataka mataifa ya Ulaya kuungana katika kupambana na janga hilo.

"Kwa wengi, hii ni Pasaka yenye upweke kutokana na huzuni na ugumu ambao janga hili lisababisha, kuanzia mateso ya kimwili hadi matatizo ya kiuchumi,” alisema, katika ujumbe uliorushwa moja kwa moja ulimwenguni kwa njia ya intaneti.

 Ametoa wito kwa "mshikamano” wa UIaya katika kupambana na virusi hivi akiongeza kuwa: "Baada ya Vita Vya Pili Vikuu vya Dunia, bara hili linalopendwa liliweza kufufuka tena.”

Nchini Uingereza, idadi ya vifo iliendelea kuongezeka na inatarajiwa kufika 10,000 hivi karibuni. Waziri Mkuu Boris Johnson anayeugua ugonjwa huo ameruhusiwa kuondoka hospitali, baada ya kulazwa kutokana na virusi vya corona Jumapili iliyopita, na kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku tatu. Ameipongeza timu ya madaktari leo kabla ya kuondoka hospitali. "Ninawashukuru sana. Wameyaokoa maisha yangu” alisema Johnson mwenye umri wa miaka 55.