1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedikt wa 16 amaliza ziara ya maeneo matakatifu

Oumilkher Hamidou15 Mei 2009

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwengu asema amani inaweza kupatikana katika eneo hilo lililotukuzwa

https://p.dw.com/p/Hr0H
Papa Benedikt wa 16 anaongoza Misa Na´zarethPicha: AP

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani,Papa Benedikt wa 16, anamalizia ziara yake katika eneo takatifu,kwa kuutembelea mji mkongwe wa Jerusalem ambako alilizuru kanisa lililojengwa mahala pale pale ambako Jesu alisulubiwa na baadae kufufuka.

Katika eneo hilo muhimu kwa waumini wa dini ya Kikristo, kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16 amesema Jesu Kristo ndie anaetoa matumaini ya amani kwa eneo la mashariki ya kati, akizungumzia uwezekano wa kukiuka vizingiti vyote vya kisasi na uhasama.

"Sisi Wakristo tunatambua kwamba amani katika eneo hili linalokumbwa na misuko suko ina jina:"Jesu Kristo", amesema Papa Benedikt wa 16, alipokua katika kanisa hilo ambako madhehebu zote za kikristo zinawakilishwa kwa mpangilio maalum.

Papa Benedikt wa 16 anasema "matunda machungu ya uhasama na visa vya kulipiziana kisasi yanaweza kuepukwa na badala yake pakachipuka mustakbal wa haki, amani, neema na ushirikiano.

Kiongozi huyo wa kanisaa katoliki ametumia muda mrefu kusali peke yake na kuomba duwa katika kanisa hilo dogo na baadae kuwasha mshumaa kama inavyotajwa katika utaratibu wa kale wa kuhiji.´

Nasaha za amani amekua akizitoa wakati wote wa ziara yake iliyoanzia Mei nane nchini Jordan. Jana Papa Benedikt wa 16 aliongoza misa kubwa kabisa huko Nazareth iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini wa kikristo.

Katika mji huo wanakoishi watu 65 elfu, thuluthi mbili kati yao ni waumini wa kiislam, kiongozi wa kanisa katoliki alisema

"Kama ulimwengu ujuavyo,kwa bahati mbaya Nazareth ulizongwa na mivutano miaka iliyopita na kuchafua uhusiano kati ya Wakristo na Waislam. Nnawatolea mwito watu wa nia njema wa jamii zote mbili wamalize uhasama wao na warejeshe imani inaytuleta pamoja ya kumuamini Mungu mmoja, baba wa walimwengu, wajenge daraja na kufungua njia ya kuishi kwa pamoja na kwa amani."

Papst Benedikt kommt in Israel an und trifft Benjamin Netanjahu
Benedikt wa 16 anajiandaa kurejea VatikanPicha: AP

Baada ya ziara yake katika kanisa lililojengwa mahala Jesu aliposulubiwa na baadae kufufuka,Papa Benedikt wa 16 anatazamiwa kukutana na mkuu wa madhehebu ya Orthodox ya Armenia kabla ya sherehe rasmi za kumuaga zitakazofanyika katika uwanja wa ndege wa Ben Gourion, karibu na Tel Aviv, na kuhudhuriwa na rais Shimon Peres na waziri mkuu Benjamin Netanyahu..

Mwandishi Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Othman Miraji