1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedikt hakutimiza matumaini ya wote

Martin,Prema/dpa26 Septemba 2011

Mada kuu katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu ni ziara ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedikt wa 16 nchini Ujerumani na uamuzi wa Vladmir Putin kugombea urais katika uchaguzi ujao.

https://p.dw.com/p/RnhF
Papst Benedikt XVI. haelt am Sonntag (25.09.11) in Freiburg im Konzerthaus eine Rede.
Papa Benedikt wa 16Picha: dapd

Basi tukianza na ziara rasmi ya siku nne ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeandika:

"Kweli Benedikt ni Papa wa Kijerumani, lakini ameitembelea Ujerumani pia kama kiongozi wa kanisa lenye kiasi ya waumini bilioni 1.2 kote duniani, akiwa na jukumu la kuhifadhi umoja na uendelezaji wa kanisa hilo. Mada kuu ya Papa ni kwamba panapokuwepo mzozo wa kanisa, hilo kwa kweli sio tatizo la taasisi bali ni tatizo la imani. Kwa maoni yake, kanisa sio mamlaka wala kampuni, bali ni zawadi ya Miezi Mungu."

Kwa maoni ya toleo la Ujerumani la FINANCIAL TIMES, Baba Mtakatifu wakati wa ziara yake hiyo nyumbani Ujerumani, hakutimiza yale yaliyotazamiwa. Linaeleza hivi:

"Kwa sehemu fulani, sababu ni kwamba matarajio yalikuwa makubwa mno: kubadili mtazamo wa kanisa kuhusu wale waliofunga ndoa nyingine baada ya kutoka kwenye ndoa ya kwanza; kuboresha dhima ya wanawake katika kuhudumia kanisa; hatua za kukabiliana na uhaba wa mapadri; maendeleo ya ekumeni - waliotaraji kupata ufumbuzi kwa yote hayo kutoka kwa Papa Benedikt hawakuitambua hali halisi. Kwani Papa Benedikt amedhihirisha kinagubaga kuwa kilicho muhimu kabisa ni kudumisha kanisa kama lilivyo. Kaulimbiu yake ni endeleeni kufuata mwongozo wa Vatican."

Na gazeti la WESTFÄLLISCHE NACHRICHTEN limeandika:

"Ni dhahiri kuwa Papa Benedikt katika umri kama wake hawezi tena kuwa mfanya mageuzi makubwa. Kwani anaelekea zaidi katika dhima ya mlinzi wa ukweli. Licha ya mtazamo huo, Benedikt katika kituo cha mwisho cha ziara yake mjini Freiburg, aliuhimza umati uliokusanyika, kuichangamsha imani yao. Amesema, imani yapaswa kuufufua ukristo na kuiendeleza mizizi yake katika familia na jamii."

926610 06/22/2011 June 22, 2011. Russian President Dmitry Medvedev, left, and Prime Minister Vladimir Putin, right, talking after laying a wreath at the Eternal Flame and the Unknown Soldier's Grave in Alexander Garden on the Day of Memory and Mourning and the anniversary of the Great Patriotic War. Sergey Guneev/RIA Novosti
Waziri Mkuu Vladimir Putin(kulia) na Rais Dmitry Medvedev wa UrusiPicha: picture alliance/RIA Novosti

Mada nyingine iliyogonga vichwa vya habari inahusika na Waziri mkuu wa Urusi, Vladimir Putin alietangaza rasmi kuwa atagombea urais katika uchaguzi ujao. Kwa maoni ya BERLINER ZEITUNG Putin na mfumo aliyounda umevuka mipaka hatari baada ya kutoa tangazo hilo.

"Ingekuwa bora kama angeendelea na wadhifa wake na kumuachia Medvedev urais. Hiyo angalao, ingewapa raia fursa ya kuendelea kuwa na matumaini ya kuona mageuzi nchini mwao. Lakini ionekanavyo, anachotaka zaidi Putin ni kujihakikishia mamlaka. Na uhakika huo unapatikana kule kwenye mamlaka. Ikiwa mageuzi katika uongozi ni jambo lisilowezekana, basi haitowezekana pia kuifanya Urusi kuwa ya kisasa."