Papa ahudhuria siku ya vijana Australia | Masuala ya Jamii | DW | 17.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Papa ahudhuria siku ya vijana Australia

Papa Benedikt wa 16 ameshtumu vikali vituo vya televisheni na mitandao ya internet kwa kutukuza vitendo vya ghasia na masuala ya ngono katika burudani.

Papa Benedict XVI, akitumbuizwa na wacheza ngoma wa Aborigine,Australia

Papa Benedict XVI, akitumbuizwa na wacheza ngoma wa Aborigine,Australia

Baba Mtakatifu Benedict wa 16 anafanya ziara rasmi ya siku 10 nchini Australia ili kuadhimisha Siku ya vijana wa Kanisa Katoliki.Lengo la siku hiyo ni kulipa kanisa katoliki muamko mpya.Mara ya mwisho sherehe hizo ziliadhimishwa mjini Cologne hapa Ujerumani mwaka 2005.Zaidi ya waumini laki mbili kutoka kote ulimwenguni wamekusanyika mjini Sydney nchini Australia.


Maelfu ya waumini walikusanyika kwenye eneo lililo nje ya jumba la tamasha la Opera ili kumuona kiongozi wa kanisa katoliki huku wakiimba pambio.Baba Mtakatifu alipita karibu na eneo hilo akiwa kwenye msafara wa maboti bandari mjini Sydney.


Kiongozi huyo ambaye ni raia wa Ujerumani aliwasili nchini Australia siku ya Jumapili.Aliwaamkia waumini hao kwa lugha yake ya kwanza -Kijerumani.


''Wapendwa nadhani munafahamu lugha yangu.Nawasalimu kutoka moyoni mwangu...munafahamu ujumbe wa furaha kutoka kwa Yesu Kristo.''

Maelfu ya vijana walikusanyika kwenye barabara za mji kumsubiri Papa Benedikt wa 16 akiwa kwenye kigari chake maalum.

Muamko mpya

Kanisa la Katoliki linataraji kuwa maadhimisho hayo yatawapa vijana muamko mpya wakati ambapo ulimwengu unakabiliwa na ubinafsi na uharibifu katika maisha ya kila siku.Muanzilishi wa siku hiyo ni marehemu Papa John Paul wa Pili.Sherehe hizo zilizoanzishwa rasmi mwaka 1986 huadhimishwa mara moja kila miaka mitatu katika miji tofauti


Hata hivyo masuala ya ulawiti na ushoga yamegubika ziara hiyo rasmi ya Baba Mtakatifu.Siku chache kabla ya kiongozi huyo wa kidini kuwasili mahakama nchini humo ilifungua upya kesi ya unyanyasaji wa kijinsia iliyowasilishwa miaka 25 iliyopita.Baba mtakatifu amesema kuwa atawaomba radhi wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia wa kanisa katoliki.Shirika la Broken Rights linalowakilisha wahanga hao limeorodhesha kesi 107 za unyanyasaji wa kijinsia na kuongeza kuwa huenda wengine bado hawajajitokeza.


Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki alilizungumzia na suala hilo alipokuwa ziarani mjini Washington,Marekani mwezi Aprili mwaka huu.Alikutana na wahanga wa kitendo hicho na kuahidi kuwafurusha wanaohusika na vitendo hivyo.

Baadhi ya wahanga wa janga hilo wanapanga kuandamana kupinga ziara ya kiongozi huyo wa kidini.Kundi hilo kwa jina ''No Pope'' linapinga mafunzo ya kanisa kuhusu ndoa na tendo lake.

Suala la Aborigine

Hapo jana Papa Benedikt wa 16 aliipongeza serikali ya Australia kwa kuomba msamaha jamii ya Aborigine kwa vitendo vya unyanyasaji walivyotendewa katika tawala zilizopita.Kiongozi huyo alisistiza umuhimu wa kudumisha maridhiano na hatua hiyo iliwapa imani jamii zinazotengwa.


''Historia ya jamii ya Aborigine ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Australia sasa.Hatua muhimu zinachukuliwa kutilia mkazo maridhjiano. kwa sasa tangu serikali ya Australia kuwatambua rasmi na kuwaomba msahama kufuatia vitendo vya unyasaji walivyotendewa awali.Mfano huu unawapa imani watu wote kote ulimwenguni ili kuhakikisha kuwa mchango wao katika jamii unaheshimiwa na kuungwa mkono ''Katika sherehe za ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya leo wachezaji wa kiasili wa Aborigine waliwatumbuiza waumini waliokusanyika bandarini wakimsubiri Papa Benedikt.


Itakumbukwa kuwa Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd aliiomba jamii ya Aborigine msamaha rasmi punde baada ya kuchukua wadhifa huo mwezi Februari.Jamii hiyo ya Aborigine ni asilimia 2 ya wakazi wote milioni 21 wa Australia.Jamii hiyo imekuwa ikitengwa na kukabiliwa na ukosefu wa kazi na unyanyasaji ikilinganishwa na raia wengine wa Australia.

Wito wa kuhifadhi mazingira

Kwa upande mwingine kiongozi huyo wa kidini aliangazia juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.Serikali ya Australia inapanga kupunguza viwango vya gesi za viwanda kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2050.Papa Benedict wa 16 alitoa wito wa kulinda mazingira ili kukilinda kizazi kijacho.


Australia inakabiliwa na kipindi kibaya zaidi cha ukame katika muda wa miaka 100.Kwa sasa inajitahidi kuokoa mito yake inayotumika kwenye kilimo.


Baba Matakatifu kadhalika alishtumu televisheni na mitandao ya internet kwa kutukuza vitendo vya ghasia na masuala ya ngono katika fani ya burudani.Alisisitiza umuhimu wa kuwa na jamii isiyounga mkono vitendo vya ghasia,iliyo na maendeleo endelevu,haki na inayojali na kuhifadhi mazingira.


Hotuba hiyo ni ya kwanza ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki tangu kuwasili nchini Australia ili kuadhimisha siku ya vijana wa kanisa katoliki.


 • Tarehe 17.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ee3V
 • Tarehe 17.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ee3V
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com