1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu Libya zaanza mazungumzo ya amani

Grace Kabogo
9 Novemba 2020

Pande mbili zinazohasimiana nchini Libya zimekutana kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, ambayo yanalenga kutafuta amani ya kudumu na kufanya maandalizi ya uchaguzi wa nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. 

https://p.dw.com/p/3l3vA
Libyen-Ägypten-Waffenruhe
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Mazungumzo hayo yanayofanyika kwenye mji mkuu wa Tunisia, Tunis yanatokana na utulivu wa miezi kadhaa uliojitokeza nchini Libya na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa mwezi Oktoba kati ya kambi mbili kuu katika mzozo huo wa muda mrefu.

Soma zaidi: Pande mbili hasimu zatia saini mkataba wa amani

Katika ujumbe wake alioutoa kwa wajumbe wakati akiufungua mkutano huo kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kuwa pande hizo zina fursa ya kuumaliza mzozo huo mbaya na kwamba ni zamu yao kuutengeneza mustakabali wa nchi yao.

"Mnaweza kuutegemea Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi zenu. Na jumuia ya kimataifa kutoa msaada wake mkubwa pia, ikiwemo kuhakikisha kikamilifu marufuku ya silaha. Mustakabali wa Libya na watu wake ni mkubwa kuliko tofauti zozote za mtu binafsi au vyama. Mustakabali wa Libya sasa uko mikononi mwenu," alisema Guterres.

Sherehe za ufunguzi wa mazungumzo hayo zilihudhuriwa pia na Rais wa Tunisia, Kais Saied.

Libya imekuwa katika vita kwa muongo mmoja tangu mwaka 2011, alipoondolewa madarakani na kuuawa Kanali Muammar Gaddafi.

New York António Guterres  UN-Konferenz zu Frauenrechten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: UN

Lakini makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Oktoba yameruhusu kuanza tena kwa uchimbaji wa mafuta na hatua iliyopigwa katika juhudi za kuumaliza mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa miaka kadhaa, lengo likiwa kuiunganisha nchi hiyo chini ya utawala mmoja na kufungua njia ya uchaguzi wa kitaifa.

Changamoto za uongozi wa mpito

Pamoja na kujiandaa na uchaguzi wa kitaifa, serikali ya mpito itakabiliana na changamoto kubwa ya kutoa huduma muhimu kwenye nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo wa kiuchumi na janga la virusi vya corona.

Umoja wa Mataifa uliwateua wawakilishi 75 wa Libya kushiriki katika mazungumzo hayo ya siku sita katika hoteli ya kifahari kwenye mji wa Gammarth, nje kidogo ya mji wa Tunis na jukumu lao kubwa ni kuhakikisha Libya inakuwa na muundo wa kisiasa, kijeshi na kijamii.

Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta kwa sasa imegawika sehemu mbili kati ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliyoko kwenye mji mkuu, Tripoli pamoja na serikali pinzani inayoongozwa na mbabe wa kivita Jenerali Khalifa Haftar iliyoko upande wa Mashariki.

Pande hizo mbili zinaungwa mkono na wanamgambo, pamoja na majeshi ya kikanda ya mataifa ya kigeni.


(AP, AFP, DPA, Reuters)