1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina kujitoa katika mkataba wa Oslo

Mjahida 1 Oktoba 2015

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amesema wapalestina hawataheshimu tena mkataba wa amani wa Oslo uliotiwa saini mwaka 1993 kati ya Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/1GgVH
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: picture-alliance/dpa/A. Gombert

Mahmood Abbas amesema Israel inaendelea kukiuka mkataba wa amani kwahiyo isitarajie Palestina kuwa upande pekee unaoheshimu mkataba huo. Mkataba huo wa Oslo uliunda mamlaka ya Palestina na kuipa Palestina utawala huru katika ukingo wa Magharibi na ukanda wa Gaza.

Hotuba ya Mahmood Abbas katika mkutano wa Umoja wa Mataifa ni dalili ya kukata tama kwa wapalestina kutokana kutopiga hatua kwa mkataba wa amani na Israel kuendelea kujenga makaazi ya walowezi wa kiyahudi.

"Kwa sasa tunatangaza kwamba hatutaendelea tena kuheshimu mikataba iliyotiwa saini kati yetu na Israel, Israel inapaswa kuwajibika."Alisema Mahmood Abbas. Kwa sasa haijawa wazi iwapo hotuba yake itasababisha mabadiliko yoyote juu ya hali halisi ya mambo ilivyo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/D. Balilty

Majadiliano ya mkataba wa mwisho wa amani ungeliifikisha palestina kuwa taifa huru lakini majadiliano hayo yalikwama mwezi Aprili mwaka wa 2014.

Abbas amesema chama cha ukombozi wa wapalestina kitachukua majukumu makubwa, akisisitiza maamuzi ya taasisi zake zinawahusu wapalestina pekee.

Waziri Mkuu wa Israel asema Abbas ndiye wa kulaumiwa

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemnyooshea kidole cha lawama Mahmood Abbas kwa kusema kuwa kiongozi huyo wa mamlaka ya wapalestina alikataa kuwa na majadiliano ya moja kwa moja naye.

Ameongeza kuwa hotuba ya Abbas katika Umoja wa Mataifa ni ya Uongo na ya kichochoezi na inaweza kusababisha mgogoro katika eneo la Mashariki ya Kati.

Aidha ofisi ya Waziri huyo mkuu wa Israel imesema inatarajia mamlaka ya wapalestaina kukubali pendekezo la Waziri mkuu kuwajibika na kuwa na majadiliano ya moja kwa moja bila masharti yoyote.

Hata hivyo waangalizi wamesema hotuba ya Abbas ni jaribio la kutaka matatizo yao kupewa kipaumbele wakati ambapo dunia inakabiliana na mambo mengine makubwa zaidi ikiwemo mgogoro wa wakimbizi, vita vya Syria, ugaidi, na mpango wa nyuklia wa Iran miongoni mwa mambo mengine.

Bendera ya Palestina ikiwa pamoja na Bendera ya Umoja wa Mataifa
Bendera ya Palestina ikiwa pamoja na Bendera ya Umoja wa MataifaPicha: Reuters/A. Kelly

Huku hayo yakiarifiwa hapo jana rais wa mamlaka ya wapalestina alipandisha bendera ya nchi yake kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa akiahidi kuwa itapandishwa pia hivi karibuni mjini Jerusalem akisema ni “mji mkuu wa Palestina”

Zaidi ya mawaziri 300 na wanadiplomasia walikuwepo katika tukio hilo, miongoni mwao akiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Saudi Arabia na Iran pamoja na mabalozi kutoka mataifa mengi ikiwemo Ufaransa. Hata hivyo Marekani ambayo haitambui taifa la Palestina haikutuma muakilishi wao katika tukio hilo.

Mwandishi: Amina Abubakar/APE/AP

Mhariri: Gakuba Daniel