Palestina yaifikisha Israel ICC | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Palestina yachukua hatua ya kihistoria

Palestina yaifikisha Israel ICC

Palestina yamtaka Fatou Bensouda kuanzisha haraka uchunguzi kamili kuhusu uhalifu wa kivita unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina. Ni baada ya kuuwawa zaidi ya Wapaletina 60 Gaza

Waziri wa mambo ya nje wa mamlaka ya wapalestina Riyad al Maliki ameitaka mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za jinai ICC kuanzisha mara moja uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita pamoja na ubaguzi unaofanyiwa Wapalestina. Ombi la Palestina limekuja wakati kukiwa na mvutano na Israeli.

Riyad al Maliki alikutana kwa muda wa saa nzima na mwendesha mashataka mkuu wa ICC Fatou Bensouda katika mahakama hiyo mjini The Hague kuizungumzia hali ya Palestina. Baadae aliwaeleza waandishi habari kwamba kikao hicho kilikuwa muhimu na hatua ya kihistoria kwa Wapalestina waliokabiliwa na mateso vizazi kwa vizazi kufuatia athari za uhalifu usiochukuliwa hatua uliofanywa na maafisa wa Israel.

 "Leo tarehe 22 mwezi Mei Mamlaka ya Wapalestina inachukua hatua muhimu na ya kihistoria kuelekea haki kwa watu wake  wanaoendelea kuteseka kutokana na uhalifu uliozagaa.Kwa niaba ya Wapalestina,Mamlaka ya Wapalestina inatumia haki yake kama watiaji saini wa makubaliano ya Roma kuifikisha hali ya Wapalestina mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya kuanzishwa uchunguzi haraka''

Ikumbukwe kwamba  ICC ilishawahi kuanzisha uchunguzi wa awali kuhusu madai ya uhalifu wa kivita na ubinaadamu,kwa upande wa Israel na Palestina lakini hakuna hatua yoyote iliyofuatia ya kuanzishwa uchunguzi kamili ambao unaweza ukasababisha kufunguliwa mashtaka.

Maliki amesema kuna ushahidi wa wazi kabisa wa uhalifu akisema kwamba wanaohusika wanapaswa kubebeshwa dhamana kwa vitendo vyao bila ya muda kupotezwa.

''Hatua hii ya kulileta hapa  suala la Wapalestina ni kipimo cha Wapalestina kwa mfumo wa Kimataifa unaohusu ubebeshaji dhamana na kuheshimu sheria za Kimataifa.''

Mkutano uliofanyika katika mahakama ya ICC umekuja baada ya kuuwawa kwa zaidi ya wapalestina 60 waliokuwa wakishiriki maandamano ya kuipinga hatua ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake kutoka Tel.Aviv kuupeleka katika mji mtukufu unaozozaniwa wa Jerusalem wiki iliyopita.

Maliki anasema hatua iliyochukuliwa hivi sasa na Palestina ya kutaka uchunguzi wa ICC imetokana na kuongezeka kwa kiwango cha uhalifu wanaofanyiwa watu wa Palestina,ikiwemo kulengwa kwa waandamanaji wasiokuwa na silaha katika ukanda wa Gaza. Kilio cha Wapalestina kinagusia pia kuhusu suala la makaazi ya walowezi wakiyahudi ambapo ujumbe wa Palestina umeyataka katika taarifa yao kwamba ni moja ya kitisho hatari zaidi kwa maisha ya Wapalestina na uhai wao.

Proteste in Gaza (DW/Y. Boechat)

Wapalestina wakiandamana Gaza

Taarifa ya ujumbe huo wa Palestina inasema  Israel inaendeleza kutanua na kuulinda utawala unaojenga  makaazi ya walowezi wakiyahudi kwa kufanya uhalifu wa kivita,uhalifu wa kibinadamu na uhalifu wa ubaguzi dhidi ya watu wa Palestina. Hata hiyo Israel sio mwanachama wa ICC na waziri wake wa mambo ya nje amesema nchi hiyo inaangalia kwa masikitiko makubwa hatua ya kufikishwa kwenye chombo hicho katika kile inachokiita hatua isiyokuwa na maana ambayo hina uhalali wowote wa kisheria.

Israel kupitia taarifa hiyo ya wizara yake ya nje imeongeza kusema kwamba ICC haina mamlaka ya kisheria katika suala la mzozo kati ya Israel na Palestina kwakuwa Israel sio mwanachama wa mahakama hiyo na kwasbabu mamlaka ya Wapalestina sio dola. Israel inamtaka Bensouda kutoshinikizwa na Wapalestina na kuzikataa zile ilizosema ni juhudi za Wapalestina za kuifanya mahakama hiyo kuwa chombo cha kisiasa.. Hata hivyo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamemtolewa mwito mwendesha mashataka mkuu Fatou Bensouda kutia msukumo wa kuendeleza hatua ya kuanzishwa uchunguzi kamili. Mashirika hayo yanasema mauaji yaliyotokea Gaza yanaonesha msisitizo wa umuhimu wa Fatou Bensouda kuchukua hatua kushughulikia  madhila wanayofanyiwa Wapalestina bila ya wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com