Pakistan yamnyonga kijana | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Pakistan yamnyonga kijana

Ulimwengu umekasirishwa na hatua ya Pakistan hivi leo kumnyonga kijana mmoja aliyetiwa hatiani kwa mauaji ya mvulana wa miaka saba hapo mwaka 2004.

Picha ya Shafqat Hussain iliyopigwa 12, Machi, 2015

Picha ya Shafqat Hussain iliyopigwa 12, Machi, 2015

Afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Pakistan, amesema kijana huyo, Shafqat Hussain, amenyongwa katika gereza la mji wa kusini mwa nchi hiyo, Karachi. Familia ya kijana huyo imevithibitishia vyombo vya habari kunyongwa kwa Shafqat. Afisa huyo amesema Shafqat amenyongwa dakika 10 hadi 12 kabla ya swala ya alfajiri.

Kaka wa Shafqat, Gul Zaman amesema katika mkutano wao wa mwisho, saa chache kabla ya kunyongwa, ndugu yake aliendelea kusisitiza kuwa hana hatia. Zaman ameliambia shirika la habari la AFP kuwa maneno ya mwisho ya kaka yake yalikuwa: ''Kamwe sikumshika huyo mvulana. Ninataka ulimwengu ulijue hilo kabla sijafa.''

Wazazi wa Shafqat Hussain

Wazazi wa Shafqat Hussain

Baada ya kuupokea mwili wa ndugu yao, kaka mwingine wa Shafqat, amedai kuwa tukio hilo halikufanyika kwa kuzingatia utaratibu unaofaa kwa sababu nusu ya shingo yake imetenganishwa na mwili wake.

Hata hivyo, familia ya kijana huyo pamoja na wakili wa familia hiyo imedai kuwa Shafqat alikuwa na umri wa miaka 14 wakati alipokutwa na hatia ya mauaji, muongo mmoja uliopita. Lakini mwezi Mei mwaka huu, uchunguzi wa serikali ya Pakistan ulihitimisha kuwa Shafqat alikuwa na umri wa miaka 23 wakati alipokamatwa mara baada ya uhalifu huo kufanyika.

Watetezi wadai kuwa Shafqat aliteswa

Watetezi wa haki za binaadamu wamedai kuwa kijana huo aliteswa ili aweze kukiri kwamba anahusika na mauaji hayo. Hukumu hiyo iliahirishwa mara nne mwaka huu ili kutatua mzozo uliokuwepo kuhusu umri aliokuwa nao kijana huyo wakati mauaji yalipotokea.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa, walielezea wasiwasi wao kuhusu kesi hiyo iliyokuwa ikimkabili Shafqat, huku wakisema haijakidhi viwango vya kimataifa. Aidha, waliihimiza Pakistan kutomnyonga kabla ya kufanya uchunguzi yakinifu wa madai kwamba aliteswa ili aweze kukiri kwamba alifanya mauaji hayo.

Watetezi wa haki za binaadamu wakipinga hatua ya kunyongwa Shafqat Hussain

Watetezi wa haki za binaadamu wakipinga hatua ya kunyongwa Shafqat Hussain

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu yamelaani vikali hatua ya kunyongwa kijana huyo. Mashirika ya haki za binaadamu yaliitaka serikali ya Pakistan kuahirisha hukumu hiyo na kuanza upya uchunguzi wa mauaji hayo, kutokana na tuhuma kwamba polisi walimtesa ili akiri kuhusika.

Disemba mwaka uliopita, Pakistan iliondoa marufuku ya kutolewa adhabu ya kifo katika kesi zinazohusiana na ugaidi, siku moja baada ya wapiganaji wa Taliban kuwaua watoto 136 katika shambulizi lililofanyika kwenye shule moja inayoendeshwa na jeshi mjini Peshawar.

Kiasi watu 180 waliohukumiwa adhabu ya kifo, wamenyongwa katika kipindi cha miezi sita, na hivyo kuifanya Pakistan kuwa nchi yenye idadi kubwa ya watu waliouawa kwa kunyongwa kwa mwaka, kama ilivyo kwa China, Iran na Saudi Arabia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,APE
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com