Pakistan yaapa kupambana na wanamgambo | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Pakistan yaapa kupambana na wanamgambo

Pakistan imesema pamoja na shinikizo la kimataifa kuitaka kuchukua hatua baada ya kutokea shambulio la kujitoa muhanga nchini India, inakusudia kuyakabili makundi ya wanamgambo.

Shambulio linalodaiwa kufanywa na Pakistan dhidi ya India linatajwa kuwaua takribani askari polisi 40 huko Kashmir mwezi uliopita. Hata hivyo waziri wa habari wa Pakistan amekanusha madai ya India na kusema nchi yake haikuhusika kwa namna yoyote na shambulio hilo la Februari 14.

Pakistan na India, zinazomiliki silaha za nyuklia zilishambuliana kwa mabomu na kujikuta katika mapigano ya anga zikipigania eneo la Kashmir linalokabiliwa na mgogoro wiki iliyopita. Nchi hizo zilisitisha mapigano hayo baada ya Pakistan kumrejesha rubani iliyemchukuwa mateka siku ya Ijumaa ikiwa ni ishara ya kutafuta amani.

Marekani na Uingereza zilipokea vyema ujio wa rubani huyo lakini ziliitaka Pakistn kuchukua hatua dhidi ya makundi ya wanamgambo yanayofanya mashambulizi katika ardhi ya India. Hata hivyo Pakistan imekanusha madai ya kuyasaidia makundi hayo ama kuyatumia kama vibaraka katika mgogoro wake na India.

Maazimio ya hapo awali ya serikali ya Pakistani kuangamiza makundi ya wapiganaji yanaoilenga India hayajazaa matunda ikiwa viongozi wa makundi ya wapiganaji hao wanaendelea kuishi kwa uhuru nchini humo. Jeshi lenye nguvu la Pakistan limekuwa likitoa maamuzi ya kiusalama na sera za kigeni ikiwa ni pamoja na uhusiano wa nchi hiyo na India.

Wanamgambo kuondolewa na kujumuishwa katika siasa

Gazeti la Dawn la nchini Pakistan linalochapishwa kwa lugha ya kiingereza lilisema kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari  vikundi hivyo vya wanamgambo vitaondoshwa hivi karibuni na kwamba vitendo vitaonekana hivi karibuni kadri mambo yanavyoendelea. Septemba 2017, Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa jeshi la Pakistan limeamua kuyabadili makundi yenye silaha ili yajiingize katika siasa.

Indien, Kaschmir, Budgam: Indische Soldaten stehen neben den Trümmern des IAF-Hubschraubers (Reuters/D. Ismael)

Wanajeshi wa India wakisimama kando ya helikopta ya jeshi iliyoanguka wilaya ya Budgam huko Kashmir 27.02.2019

Mbinu hiyo imekosolewa vikali na makundi ya kijamii na serikali iliyopita baada ya kujitokeza kwa chama kipya kinachohusishwa na Hafiz Saeed, anayetuhumiwa kusuka mpango wa shambulio la Mumbai la mwaka 2008 lililoua watu 166. Saed alikanusha kuhusika na tukio hilo lakini chama hicho kipya kilipigwa marufuku.

Hata hivyo waziri wa habari, Fawad Chaundry, alisema Pakistan ingetumia mkakati wa kiuchumi na kisiasa  ambao ungezingatia mpango wa kitaifa wa mwaka 2014 wa nchi hiyo ulioapa kuyaondoa makundi ya wapiganaji.

Waziri huyo aliongeza kuwa nchi yake ingetimiza matakwa ya Shirika la Kimataifa linalofuatilia masuala ya Uchumi la Financial Action Task Force, FATF, ambalo mwaka 2018 liliitaja Pakistan katika orodha ya nchi zinazojihusisha na ugaidi, baada ya kuombwa lifanye hivyo na Marekani na Umoja wa Ulaya. Chandry alisema serikali yake inakusudia kudhibiti mianya yote ambayo inaruhusu makundi yaliyopigwa marufuku kuendelea na shughuli zake na kuongeza kuwa changamoto kubwa inayoikabili serikali yake ni makundi hayo kubadili majina jambo ambalo ni la kushughulikiwa.

Wiki iliyopita, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilipendekeza kwa baraza la Umoja wa mataifa kumweka kwenye orodha ya watu wanaofuatiliwa kwa karibu, kiongozi wa kundi la JeM, Masoos Ahzar, pendekezo litakalopigiwa kura katikati ya mwezi Machi likimlenga mshirika wa Pakistan, China ambayo hapo awali ilizuia jaribio la kumwekea vikwazo kiongozi huyo wa kundi la JeM.

Jumanne iliyopita, India ilishambulia kambi inayodaiwa kuwa ya mafunzo na kuua magaidi wengi. Hata hivyo Pakistan imekanusha kuwepo kwa kambi hiyo na kuwaalika waandishi wa habari kutembelea eneo la tukio. Kwa upande wao wanakijiji wa mahali hapo walisema hakuna shughuli zilizokuwa zikiendelea katika eneo hilo ingawa waliinyoshea kidole madrasa iliyo jirani inayotajwa kumilikiwa na kundi la wapiganaji la JeM.

reuters

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com