1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan: Marekani imepotosha mazungumzo ya Pompeo na Khan

Sudi Mnette
24 Agosti 2018

Pakistan imeitaka Marekani kurekebisha, ilichokiita kama "maelezo yasiyo sahihi" baada ya kunukuu mazungumzo ya simu kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo na waziri mkuu mpya wa Pakistan Imran Khan

https://p.dw.com/p/33ghL
Mike Pompeo
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike PompeoPicha: picture-alliance/dpa/Yonhapnews Agency

Hayo yanaibuka katika kipindi kifupi kabla ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo mjini Islamabad, ambayo imepangwa kufanyika wiki ya kwanza ya mwezi ujao. Lengo la ziara hiyo ni kukutana na Waziri Mkuu Imran Khan, ambae alianza kutumikia wadhifa huo wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na wizira ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, inasema Pompeo alizungumza na Khan kwa njia ya simu na kumtakia mafanikio mema, na pia kumtaka achukue hatua madhubiti dhidi ya makundi yote ya kigaidi yanayoendeshwa kutoka katika ardhi ya Pakistan. Kwa kawaida maafisa wa Marekani huibua suala la Taliban na makundi mengine ambayo yanaendesha shughuli zao katika maeneo salama nchini Pakistan na kupanga mashambulizi dhidi ya Marekani na majeshi ya Afghanistan katika eneo la mpakani.

Pakistan yasisitiza Wataliban hawapangi mapigano katika ardhi yake.

Pakistan - Imran Khan ist der neue Ministerpräsident
Waziri Mkuu mpya wa Pakistan Imran KhanPicha: picture-alliance/Photoshot

Pakistan pia kwa upande wake imekuwa ikikanusha kwamba Wataliban wanapanga mashambulizi katika ardhi yake. Na usiku wa Alhamis, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan ilidai kwamba suala la makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu halikugusiwa kabisa katika mazungumzo ya simu kati ya Pompeo na Khan.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa kupitia mtando wa Twitter msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Pakistan aliandika kuwa: "Pakistan inauchukuliwa kwa namna ya kipekee upotoshaji uliotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu mazungumzo ya simu ya leo." Maandishi hayo yaliendelea kufafanua " Kwa ujumla hakukutajwa suala lolote linalohusu magaidi wanaoendesha shughuli zao nchini Pakistan. Upotoshaji huo unapaswa kurekebishwa haraka."

Kauli ya Marekani kuhusu lawama za upotoshaji

Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Heather Nauert, alionesha kutokuwa na ishara yoyote ya kufanyika marekebisho ya tuhuma hizo. Nauert aliwaambia waandishi wa habari kwamba Pakistan ni mshirika muhimu katika ukanda. Alisema Pompeo alifanya mazungumzo mazuri na waziri mkuu mpya na wanatarajia uwepo wa ushirikino mzuri katika siku za usoni.

Pompeo anatarajiwa kuwasili nchini Pakistan Septemba 5, na anaweza kuwa kiongozi wa kwanza muhimu na wa ngazi ya juu kabisa kuonana na Waziri Mkuu Khan tangu alipoapishwa.

Waziri Mkuu Khan amekiwsha onesha ushirikiano anaoutaka na Marekani aliposema "Tutatafuta suluhisho la kisiasa. Tungalipenda kujifungamanisha na amani na Marekani. Ni muda wa kutoa nafasi kwa amani kwa pamoja kati ya Pakistan na Marekani. Tumechoshwa na mapigano."

Khan anafahamika vyema kwa ukosoaji wake wa sera ya kijeshi ya Marekani nchini Afghanistan, ingawa juma lililopita baada ya kushinda uchaguzi wiki iliyopita alisema kwamba atatafuta mahusiano bora na Marekani, baada ya mkururo wa misaada kusitishwa na kusitishwa kwa mafunzo ya kijeshi ya Marekani.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR

Mhariri:Iddi Ssessanga