1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Pakistan:Kuondolewa kwa Khan kutaleta utulivu au mzozo mpya?

Iddi Ssessanga
12 Aprili 2022

Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan anaacha nyuma historia ya ukosefu wa utulivu wa kiuchumi na kisiasa. Wapinzani wake wa kisiasa ambao sasa wanashikilia mamlaka wanaahidi mageuzi, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa.

https://p.dw.com/p/49rEW
Prime Minister Shahbaz Sharif
Picha: National Assembly of Pakistan/AP/picture alliance

Kufuatia kuondolewa kwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan katika kura ya kutokuwa na imani naye, wataalam wanasema mabadiliko ya kisiasa yanaweza kuleta utulivu wa muda mfupi, lakini uongozi mpya hivi karibuni utakabiliwa na changamoto zilizorithiwa kutoka serikali ya zamani.

Khan alikuwa amejaribu kukwepa kura ya kutokuwa na imani naye karibu wiki mbili zilizopita kwa kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya, na hivyo kuzua mgogoro wa kikatiba.

Soma zaidi: Sharif achaguliwa waziri mkuu mpya Pakistan baada ya kuondolewa Khan

Mahakama ya Juu ya Pakistan iliitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha katiba siku ya Alhamisi, na kuwaamuru wabunge wakutane tena.

Siku ya Jumatatu, Bunge lilimchagua kiongozi wa upinzani Shahbaz Sharif kuwa waziri mkuu mpya wa Pakistan. Sharif ni rais wa chama cha mrengo wa kati cha Pakistan Muslim League - Nawaz.

Upinzani Pakistan washerehekea

Baada ya kura ya Jumapili ya kutokuwa na imani naye, makumi ya wanachama wa chama cha upinzani waliingia mitaani kuonesha furaha yao.

"Leo, ninaipongeza nchi nzima," alisema Maulana Fazalur Rehman, mkuu wa muungano wa upinzani wa Pakistan Democratic Movement (PDM). "Huu ni ushindi wa katiba yetu na taifa zima," aliongeza.

Pakistan Imran Khan TV Ansprache
Watu wakimsikiliza aliekuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan wakati akilihutubia taifa Machi 8, 2022, mkesha wa kura ya kutokuwa na imani naye.Picha: Aamir Qureshi/AFP

"Huu ni wakati muafaka kwa historia ya kikatiba ya Pakistan," Shahid Khaqan Abbasi, waziri mkuu wa zamani, aliiambia DW.

Shahbaz Sharif aliwaambia waandishi wa habari kwamba ilikuwa siku muhimu kwa nchi.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Pakistan akabiliwa na kura ngumu ya kutokuwa na imani naye

"Muungano huu utaijenga upya Pakistan, na hatutajiingiza katika unyanyasaji wa kisiasa wa wapinzani," alisema baada ya kura ya Jumapili.

Wafuasi wenye hasira wa chama cha Khan cha Tehreek-e-Insaf (PTI) walipiga kelele dhidi ya Marekani kufuatia kuondolewa kwake. Khan alikuwa ametoa madai yasiyothibitishwa kwamba Marekani ilishirikiana na vyama vya upinzani kumuondoa.

Khan alikuwa ameitisha maandamano dhidi ya kile alichokiita jaribio la "kuweka" serikali mpya na "mamlaka za kigeni." Iliwalaazimu polisi wa kutuliza ghasia kuingilia kati na kutenganisha pande hizo.

Nini kinafuata kwa Pakistan?

Baadhi ya wachambuzi na wataalamu wa sheria wanasema kuondolewa kwa Khan ni ushindi wa katiba na demokrasia nchini Pakistan. Hata hivyo, iwapo serikali mpya italeta utulivu ni swali lililo wazi.

"Uamuzi huu umeleta ushindi mkubwa kwa demokrasia na katiba ya Pakistan, na inaeleweka kuwa upinzani unafurahi kwamba sasa utakuwa na nafasi ya kuchukua mamlaka," Michael Kugelman, mtaalam wa Asia Kusini katika Kituo cha utafiti cha Woodrow Wilson chenye makao yake mjini Washington, Washington. aliiambia DW.

Pakistan Protest nach Misstrauensvotum gegen Imran Khan | Karachi
Chama cha Imran Khan cha PTI kitandelea kuwa nguvu kubwa katika siasa za Pakistan.Picha: Rizwan Tabassum/Getty Images/AFP

"Lakini, baada ya furaha hiyo kupungua, kuna uwezekano wa kutokea mwamko mbaya. ... Itarithi hali mbaya ya kiuchumi," alisema.

Chini ya Khan, Pakistan ilitumbukia kwenye mgogoro wa kiuchumi, ambapo mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira viliongezeka pakubwa.

Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kumezidisha matatizo ya kiuchumi ya Pakistan, huku sarafu yake ya rupia ikiporomoka hadi chini kabisa dhidi ya dola ya Marekani siku ya Alhamisi.

"Dola ya Marekani inapoendelea kupanda, mdororo mkubwa wa kiuchumi unaitazama nchi," Sharif aliandika kwenye Twitter.

"Uamuzi wa mahakama unairejesha Pakistan kwenye mkondo wa kuwa na serikali inayofanya kazi. Hii ni ishara nzuri kwa masoko ambayo yalikuwa yanasuasua kutokana na kutokuwa na uhakika katika siku za hivi karibuni. Lakini njia ya utulivu bado ni ndefu," mtaalamu wa masuala ya kiuchumi Khurram Husain, aliiambia DW.

Soma pia: Pakistan yaandaa mkutano kujadili kadhia ya Afghanistan

"Serikali mpya inapaswa kuingia, na kutafuta haraka njia za kuanzishwa tena kwa mpango wa IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa), na kwa njia hiyo inapaswa kufanya maamuzi magumu yanayohitajika ili hili lifanyike. Njia iliyo mbele yetu si rahisi," lakini angalau inafunguka sasa,” alisema Husain.

Wataalamu wengine wanasema kuondolewa kwa Khan kunaweza kuzusha duru mpya ya machafuko ya kisiasa katika taifa hilo lenye historia ya uingiliaji wa kijeshi katika siasa.

Pakistan Protest nach Misstrauensvotum gegen Imran Khan | Peshawar
Wafuasi wa Khan wakinadamana kupinga kuondolewa kwake.Picha: Abdul Majeed/Getty Images/AFP

Pakistan imeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi tangu ilipojitangazia uhuru wake mwaka 1947.

Ushindi wa kikatiba kwa Pakistan?

Mtaalamu wa sheria Osama Malik aliiambia DW kuwa mahakama ya Katiba kimsingi ilizuwia mapinduzi ya kiraia.

Soma pia:Imran kumwita Osama shahid ni kuteleza ulimi?

"Katika mfumo ambapo utatu wa madaraka upo, mhimili wa mtendaji unaposhambulia bunge, inakuwa ni jukumu la mahakama kulinda bunge. Jaji mkuu na majaji wenzake wametimiza wajibu huo na kutoa msaada kwa demokrasia changa ya Pakistan. " alisema.

Atika Rehman, mwandishi wa habari wa gazeti la Dawn la Pakistan, aliiambia DW kwamba hatua ya mahakama ya juu kuamuru kura ya kutokuwa na imani ni "uamuzi wa kihistoria" ambao ulishikilia "ukuu" wa katiba ya Pakistan.

"Katika siku za nyuma, kulikuwepo na sura za giza ambazo zimekuwa doa katika demokrasia yetu. Mahakama ilithibitisha kwamba siku hizo ni za zamani. Ni uamuzi unaokaribishwa sana," aliongeza.

"Changamoto kwa waziri mkuu mpya ni kubwa na yenye pande nyingi," Rehman alisema.

"Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kutasababisha mdororo zaidi wa kiuchumi, na, kwa kuwa bei za bidhaa tayari zimepanda kuliko wakati mwingine wowote, inaweza kusababisha machafuko ya umma," Rehman aliongeza. "Hali inazidi kuwa ngumu na inahitaji hatua za haraka na za kuona mbali ili kuwapa unafuu wananchi."