1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan katika mzozo zaidi wa kisiasa

Ponda, Eric Kalume26 Agosti 2008

Ikiwa imesalia majuma matatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Pakistan, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa nchini hiyo Pervez Msharraff, siasa nchini humo zimeanza kupamba moto.

https://p.dw.com/p/F51X
Mwenyekiti wa Chama cha Pakistan Peoples Party anayewania Urais wa Pakistan, Asif Ali ZardariPicha: AP

Tayari kiongozi wa chama cha Pakistan People Party PPP, ambaye ni mume wa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo aliyeuawa Benazir Bhutto, Asif Ali Zardari, amewasilisha makaratasi yake ya uteuzi kuwania kiti hicho cha Urais wakati wa uchaguzi  utakapoitishwa  hapo Septemba 6 mwaka huu. 


Chama hicho cha PPP  kinapigiwa upato kushinda uchaguzi huo, baada ya kushinda viti vingi bungeni wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Februari mwaka huu.


Zardari  ambaye alichukua hatamu ya uongozi wa chama hicho kufuatia shambulizi la bomu  lililomuua mkewe Benazir Bhutto Mwezi Desemba mwaka uliopita, anaamini chama chake cha PPP kitapata ushindi mkubwa wakati wa uchaguzi huo kutokana na kwamba kinaungwa mkono na idadi kubwa zaidi ya wabunge inayohitajika bungeni.


 Aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Nawaz Shariff ambaye chama chake kimejitoa katika serikali ya mseto siku ya Jumatatu, kufuatia mzozo wa ndani katika serikali hiyo ya Mseto, kuhusu kurejeshwa nyadhifani kwa majaji walioachishwa kazi, pia  amemteua jaji Mstaafu wa mahakama kuu Saeed Uz Zaman Siddiqui kupambana na Zardari.


Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu  kwa Rais Pervez Musharraf, kufuatia   shinikizo kutoka kwa  vyama mseto  katika serikali hiyo ya muungano, la kutaka kumshtaki kwa kutumia vibaya mamlaka yake.


Chama cha Pakistan Muslim League ambacho kilimuunga mkono Musharraf, kwa upande wake kimemteua katibu mkuu, Mushahid Hussain, kuwania wadhifa huo.


 Wakati huo huo  afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani nchini Pakistan amenusurika kifo baada ya kufyatuliwa risasi  katika eneo la kaskazini magharini mwa Pakistan.


Maafisa  wa usalama nchini himo wanasema kuwa  Nancy Tracy alishambuliwa kwa  bunduki aina ya AK 47 alipokuwa akitoka katika ofisi za ubalozi mdogo  wa Marekani Mjini Peshawar.


Aidha katika tukio jingine watu wasiopungua 20 wamejeruhiwa kufuatia mlipuko uliotokea katika jimbo la Baluchistan lenye utajiri mkubwa wa mafuta.Visa vya ghasia vimeongezeka nchini humo huku viongozi wake wa kisiasa wakizozana kisiasa.