Paetongtarn Shinawatra achaguliwa Waziri Mkuu mpya Thailand
16 Agosti 2024Paetongtarn, mwenye umri wa miaka 37, na mtoto wa kiongozi wa zamani wa Thailand, Thaksin Shinawatra, ndiye kiongozi mdogo kabisa kuwahi kuchaguliwa katika historia ya nchi hiyo.
Kama mgombea pekee, Paetongtarn aliidhinishwa Ijumaa kwa kura 319, huku wabunge 145 wakipiga kura kumpinga, na wabunge 27 hawakupiga kura.
Uchaguzi ulikuwa wa wazi hadharani
Akitangaza matokeo hayo, Spika wa Bunge, Wan Muhamad Noor Matha alisema wabunge walitumia takriban saa moja kupiga kura zao hadharani mmoja baada ya mwingine.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo wa bunge, Paetongtarn kiongozi wa chama tawala cha Pheu Thai, alielezea kufurahishwa kwake na uamuzi huo wa bunge, kwa sababu hiyo ni heshima kubwa sana kwake.
"Nimefurahi sana leo. Kwa kawaida, huwa napanda jukwaani mara nyingi sana, na huwa sipatwi na msisimko kabisa, lakini leo ni kama mikono yangu inatetemeka. Najaribu kuwaambia jinsi ninavyojisikia hivi sasa. Sahamani kwa hilo," alifafanua Paetongtarn.
Akizungumza na waandishi habari baada ya kuthibitishwa na bunge, waziri mkuu huyo mteule amesema ana matumaini ataweza kuwafanya wananchi wajiamini, ataboresha hali ya maisha na kuwawezesha wananchi wote wa Thailand. Amesema ana matumaini anaweza kufanya kila awezavyo kuifanya nchi hiyo isonge mbele.
Paetongtarn anasubiri kupata ridhaa ya kifalme
Paetongtarn atakuwa rasmi Waziri mkuu baada ya kupewa ridhaa ya kifalme, ingawa bado siku rasmi ya kuidhinishwa haijatangazwa.
Paetongtarn anakuwa kiongozi wa tatu wa Thailand kutoka katika familia ya Shinawatra, baada ya baba yake Thaksin Shinawatra ambaye aliondolewa katika mapinduzi, kabla ya kurejea kutoka uhamishoni mwaka uliopita, na pia shangazi yake Yingluck Shinawatra ambaye bado anaishi uhamishoni.
Waziri Mkuu aliyepita, Srettha Thavisin aliondolewa madarakani na Mahakama ya Katiba siku mbili zilizopita, kwa madai ya kukiuka maadili. Paetongtarn amesema amesikitishwa na hatua ya kuondolewa Srettha, na hivyo akaona ni wakati sahihi kufanya jambo kwa ajili ya nchi yake na chama chake. Anasema ameufikia uamuzi huo baada ya kuzungumza na Srettha, familia yake na watu wa chama chake.
Changamoto zinazomkabili Paetongtarn
Waziri mkuu huyo mteule anakabiliwa na kibarua kikubwa cha kufufua uchumi wa Thailand na kuepuka mapinduzi ya kijeshi na uingiliaji kati wa mahakama, ambao umeondoa utawala wa awamu nne zilizopita. Hata hivyo, Paetongtarn amesema serikali yake itakuwa imara kwa sababu ana timu yenye uzoefu.
Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Manet, amemtumia Paetongtarn salamu za pongezi baada ya kuchaguliwa kwake.
(AP, AFP, Reuters)