1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oxfam yasema mabilionea wananufaika kuliko kada masikini

Isaac Gamba
22 Januari 2018

 Katika kuelekea kongamano la kimataifa la kujadili uchumi wa dunia, shirika la misaada la Oxfam limesema kuwa utafiti wake unaonesha kuwa asilimia 82 ya kipato kilichokusanywa  mwaka jana kilikwenda kwa matajiri.

https://p.dw.com/p/2rHWu
Andres Gonzalez Rodriguez Oxfam
Picha: Mohammed-Ali Abunajela/ Oxfam

 Shirika hilo la misaada la Oxfam limeamua kuonyesha tofauti ya kipato iliyopo kati ya masikini na matajiri ikiwa ni kabla ya kuanza kwa  kongamano la kimataifa la masuala ya uchumi linalofanyika mjini Davos Uswis.

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika hilo  inaonesha katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010  mabilionea wakiongezeka kwa haraka zaidi huku kada ya wafanyakazi wa kawaida wakizidi kuwa masikini.

Oxfam imetumia matokeo ya utafiti wake kuonyesha picha halisi ya hali ya uchumi duniani  ambapo jamii ya watu matajiri inazidi kukuwa kiuchumi mnamo wakati mamilioni ya watu wakiendelea kupambana na hali ya umasikini kutokana na kulipwa ujira mdogo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Oxfam Winnie Byanyima ametahadharisha katika taarifa yake  kuwa ongezeko la mabilionea duniani si ishara  ya kukuwa kwa uchumi duniani bali ni dalili inayoonesha kuanguka kwa uchumi.

Oxfam  imebainisha kuhusiana na hali ya kipato kwa jamii ya wanawake wafanyakazi  ambao kwa mujibu wa utafiti huo wanaendelea kupata kipato kidogo kuliko wanaume na kuongeza kuwa mara nyingi wanawake wamekuwa wakifanya kazi ambazo mshahara wake ni mdogo huku shirika hilo likisema mabilionea tisa kati ya kumi ni wanaume.

Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari kisemacho "zawadia kazi na siyo utajiri" ilitumia takwimu zilizopo zinazohusu  mapato wanayopata watendaji wakuu pamoja na wenye hisa katika taasisi  na mashirika mbalimbali  kulinganisha na mapato ya wafanyakazi wa kawaida.

 

Kipato cha watendaji wakuu ni kikubwa sana kulinganisha na cha wafanyakazi wa kada ya kati

Südafrika | World Economic Forum on Africa 2017 | Winnie Byanyima
Mkurugenzi mtendaji wa Oxfam,Winnie Byanyima Picha: World Economic Forum/J. Polacsek

Oxfam katika ripoti yake imetolea mfano wa kipato ambacho baadhi ya watendaji wakuu wa makampuni wanakusanya kwa siku nne ndicho ambacho mfanyakazi katika sekta ya kiwanda cha kutengeneza nguo nchini Bangladesh anapata katika kipindi chote cha maisha yake.

Byanyima, Mkurugenzi mtendaji wa Oxfam amesema  watu wanaotengeneza nguo, kuunganisha vifaa katika viwanda  vya simu pamoja na kuzalisha mazao ya chakula  wanatumikishwa  kwa manufaa ya kutengeneza faida ya makampuni yaliyowaajiri pamoja na kuongeza utajiri wa mabilionea.

Ili kukabilina na tofauti kubwa ya kipato kati ya kundi la jamii ya watu masikini na wale walio matajiri  shirika la Oxfam limetoa mwito wa serikali kufuatilia kwa makini vipato wanavyopata watendaji wakuu pamoja na wenye hisa katika mashirika mbalimbali  ikiwa ni pamoja na kudhibiti ukwepaji wa kodi kama ilivyoelezewa katika machapisho ya hivi karibuni ya Panama Papers na Paradise Papers.

Aidha imesema kuna haja ya  kuongeza bajeti katika sekta ya afya na elimu.

Ripoti ya utafiti huo imetolewa mnamo wakati wanasiasa wa ngazi ya juu na wafanyabiashara wakubwa wakitarajiwa kukutana katika kongamano la kimataifa la masuala ya uchumi nchini Uswisi  ambalo mwaka huu litaangazia jinsi ya kuwa na jamii inayonufaika na kile kinachozalishwa.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/ape

Mhariri: Iddi Ssessanga