1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mhasibu wa Auschwitz miaka minne gerezani

Mjahida15 Julai 2015

Mahakama ya Ujerumani imemhukumu miaka minne jela kachero wa Zamani Oskar Groening, baada ya kupatikana na hatia ya kutoa ushirikiano wake, katika mauaji ya wanazi 300,000 kwenye kambi ya Auschwitz-Birkenau.

https://p.dw.com/p/1Fz0J
kachero wa Zamani Oskar Groening
kachero wa Zamani Oskar GroeningPicha: Reuters/A. Heimken

Kesi ya Groening, aliye na miaka 94, ambaye mara kwa mara hufahamika kama mhasibu wa Auschwitz, inatarajiwa kuwa moja ya kesi za mwisho dhidi ya wanazi wa zamani nchini Ujerumani kufuatia wengi wa walioshitakiwa kuwa wameaga dunia.

Korti ya mji wa Lueneburg kaskazini mwa Ujerumani ilimkuta na hatia kachero huyo wa zamani kwa kuhusika na mauaji ya wayahudi 300,000 katika kambi kubwa ya maangamizi nchini Poland wakati ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na wanazi miaka 70 iliyopita. Zaidi ya watu milioni moja waliuawa katika kambi hiyo wengi wao wakiwa wayahudi, watu 7,000 pekee ndio walionusurika.

Kwa sasa waendesha mashtaka wa taifa wanapaswa kuamua iwapo Groening anaweza kweli kutumikia kifungo chake kwa kuangalia miaka yake, pamoja na afya yake.

Katika miezi minne ya kesi hiyo, korti ilisikiliza ushahidi wa kuogofya kutoka kwa manusura waliokuwepo katika kambi hiyo na kutoka kwa Groening mwenyewe, aliyeelezea namna kachero mmoja wakati huo alivyombamiza kwa nguvu mtoto mchanga pembezoni mwa gari wakati alipokuwa akilia.

Oskar Groening akiwa pamoja na mawakili wake wakati wa kusikilizwa kwa kesi dhidi yake mjini Lueneburg, Ujerumani
Oskar Groening akiwa pamoja na mawakili wake wakati wa kusikilizwa kwa kesi dhidi yake mjini Lueneburg, UjerumaniPicha: Reuters/A. Heimken

Katika ushahidi wake Groening alisisitiza kuwa ni mara mbili tu au tatu alipokuwa katika kambi hiyo ya Auschwitz ambapo wafungwa wapya waliowasili, walikaguliwa na kujulikana ni kina nani waliokuwa katika hali nzuri ya kufanya kazi ngumu na kina nani wanaopaswa kuuwawa kwenye vyumba vya gesi ya sumu.

Baraza la Wayahudi lapongeza kifungo cha Oskar Groening

Aidha rais wa Baraza la Wayahudi duniani Ronald S. Lauder ameupongeza uamuzi wa mahakama ya Ujerumani, akisema haki imepatikana, huku akiongeza kuwa bwana Groening alikuwa mtu mdogo sana katika kambi hiyo lakini bila ya mchango wa watu kama yeye mauaji ya mamilioni ya wayahudi yasingetokea.

Hata hivyo Oskar Groening hakuwahi kukataa makosa aliyoyafanya wakati huo, alikubali kushiriki mauaji hayo katika siku ya kwanza ya kusikilizwa kesi yake. Lakini katika taarifa yake aliyoiandika mwenyewe Groening, alisema hawezi kuwauliza manusura wa mauaji ya halaiki ya wayahudi katika vita vya pili vya dunia kumsamehe, kwa sababu haoni kama anastahili msamaha huo kutokana na mateso waliyoyapata.

"Naweza tu kumuomba Mungu anisamehe," aliandika Groening katika taarifa yake.

Oskar Groening alipokuwa na miaka 21 aliamua kujiunga na jeshi la makachero kabla ya kusajiliwa mwaka wa 1942 kufanya kazi katika kambi ya Auschwitz, ambapo alihesabu pesa zilizopatikana katika mizigo ya wafungwa na kutuma pesa hizo katika makao makuu ya askari kanzu mjini Berlin.

Oskar Groening akiwasili mahakamani mjini Lueneburg, Ujerumani
Oskar Groening akiwasili mahakamani mjini Lueneburg, UjerumaniPicha: Reuters/F. Bimmer

Mashtaka dhidi ya Groening yanahusiana na kipindi kati ya mwezi Mei na Julai mwaka wa 1944 wakati magari ya moshi yaliyokuwa yamewabeba mayahudi yalipowasili katika kambi ya Auschwitz, kutoka Hungary. Takriban 300,000 kati yao waliuwawa ndani ya vyumba vya gesi.

Kwa miongo kadhaa amekuwa akiishi maisha ya kawaida katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Lueneburg, ambapo alifanya kazi katika kiwanda cha glasi, na kuishi pamoja na mkewe na watoto wake baada ya kuachiwa kutoka gereza moja nchini Uingereza muda mfupi baada ya kumalizika vita vya pili vya dunia.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri Josephat Charo