Opereshini za Polisi dhidi ya magaidi wa itikadi kali za kidini nchini Moroko | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Opereshini za Polisi dhidi ya magaidi wa itikadi kali za kidini nchini Moroko

Magaidii watuhumiwa wajiripua kukwepa wasikamatwe na polisi huko Casablanka

Wafuasi wane wa kundi la wenye kujiripua wanaotuhumiwa kuandaa mashambulio ya kuyatolea mhanga maisha wameshindwa nguvu jana mjini Casablanka ambako watatu kati yao walijiripua na wanne kuuliwa na polisi.

Alipojiripua jana usiku,mwanaharakati huyo wanne wa kigaidi aliwajeruhiwa watu wasiopungua 19,wakiwemo askari polisi watano.

Watuhumiwa wawili walikua wakisakwa mtindo mmoja na polisi tangu opereshini ilipoanzishwa alfajiri ya jana katika nyumba moja ya mtaa wa madongo poromoka huko Fida,ambapo gaidi mmoja mtuhumiwa aliuliwa na polisi na mwengine alijiripua akiwa juu ya paa la nyumba hiyo.

Mtu watatu wa kundi hilo hilo alijiripua jioni alipodhania amefanikiwa kuwakwepa polisi waliokua wameuzingira mtaa mzima ili wamkamate.

Askari polisi mmoja ameuwawa na mwengine kujeruhiwa mtuhumiwa huyo alipojiripua si mbali na mahala polisi walipokuwepo.

Shirika la habari la Moroko-MAP linamtaja mwanaharakati huyo watatu aliyejiripua kua ni Rachidi Mohammed aliyekua mfuasi wa kundi la magaidi wanaotuhumiwa kuhusika na kuuliwa mwanajeshi mmoja wa Moroko mnamo mwaka 2003.

“Wanne amejiripua alipoona hana pa kupita”-duru za vikosi vya usalama zimesema na kushadidia mtu huyo wanne alikua wa mwisho kati ya waliokua wakisakwa na polisi katika opereshini hiyo.

Askari polisi mmoja anasema lengo la mwanaharakati huyo lilikua kusababisha hasara kubwa zaidi ya maisha,na hasa miongoni mwa vikosi vya usalama.

“Alikiuka eneo lililotengwa na polisi na kujipenyeza katika kundi la wambeya na waandishi habari ili kuwajongelea askari polisi na kujiripua”-askari polisi huyo ameongeza kusema.

Viongozi wa Maroko wako katika hali ya tahadhari tangu wanaharakati 13 wa itikadi kali walipojiripua mwaka 2003 katika eneo la kati la mji mkuu wa kiuchumi Casablanka na kuangamiza maisha ya watu 32 wengine.

Tangu mwezi mmoja uliopita polisi wamekua wakiwaandama wanaharakati dazeni moja hivi wa kundi la wenye kujiripua ,wanaotuhumiwa kuandaa mashambulio dhidi ya meli za kigeni katika bandari ya Casablanka na dhidi ya vituo vyengine vya watalii katika mji huo.

Wanaharakati wote wanne waliouwawa jana wanasemekana ni miongoni mwa wafuasi wa kundi hilo.

Duru za polisi zinasema watuhumiwa hao walidhamiria kusalia na mikanda yao ya miripuko hadi wangekamtwa na polisi.

Mamia ya watu walifika karibu na nyumba iliyokua imelengwa kuvamiwa na polisi huku wataalam wakichunguza kama wanaharakati hawajazika miripuko ndani ya nyumba hiyo.

Vikosi vya usalama vinasema vinaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wa kigaidi wanaohofiwa wamejificha mjini Casablanka.

Wanaharakati hao wa kigaidi wanadai wanataka kuwaadhibu wamoroko kwasababu ya ushirikiano wa nchi hiyo na Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi.

 • Tarehe 11.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGZ
 • Tarehe 11.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGZ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com