Operesheni za manuwari ya Kijerumani katika Pembe ya Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Operesheni za manuwari ya Kijerumani katika Pembe ya Afrika

Manuwari "Mecklenburg Vorpommern" katika pembe ya Afrika

Wanajeshi wa Kijerumani katika manuwari huko Pembe ya Afrika

Wanajeshi wa Kijerumani katika manuwari huko Pembe ya Afrika

Tangu pale Jumuiya ya Kujihami ya NATO ilipotangaza kwamba nchi za jumuiya hiyo zitaidiana kijeshi katika maeneo ya hatari, na mchango wa Ujerumani ukaamuliwa utolewe katika ile operesheni inayoitwa Enduring Freedom, jeshi la Ujerumani limekuwa likishiriki kupambana na ugaidi katika eneo la Pembe ya Afrika. Tangu wakati huo, wanajeshi na mabaharia wa Kijerumani wamekuweko katika anga na bahari ya eneo lililo kubwa mara nane ya Ujerumani. Walichogundua ni shehena ndogo za silaha na madawa ya kulevya. Muda wa kuweko wanajeshi hao katika eneo hilo ulirefushwa hapo tarehe 13 mwezi huu, lakini idadi ya wanajeshi hao imepunguzwa kufikia 800.


Tangu wiki hii, manuwari ya Kijerumani ilio na jina la Mecklenburg Vorpommern imekuwa tena njiani katika Pembe ya Afrika ambako maharamia wa Kisomali wamelifanya eneo hilo kuwa lisilokuwa na usalama. Wakati wanasiasa mjini Berlin wanabishana namna gani na kwa uwezo gani Ujerumani inaweza kushiriki katika mapambano dhidi ya maharamia wa baharini waliojizatiti, kisilaha, hofu zinazidi miongoni mwa mabaharia juu ya uwezekano wa kutokea mapigano baharini. Ludgar Scherdomsky alikuweko kwa siku moja katika manuwari ya Mecklenburg Vorpommern na akapata sura vipi mabaharia wanavoyachukulia majadiliano yanayoendelea mjini Berlin.

Ni saa tano za mchana mjini Jibuti na ni zaidi ya nyuzi joto 30 katika kipimo cha Celsius pale manuwari ya Mecklenburg-Vorpommern, ikichelewa kwa saa moja, mwishowe iliweza kupandisha nanga. Nahodha Kay-Achim Schönbach wa manuwari hiyo alisema kwanza wataelekea eneo la Ghuba ya Aden, karibu na mpaka wa Yemen, ili kuendeleza kampeni yao dhidi ya ugaidi wa kimataifa, na baadae wataelekea pembezoni mwa mwambao wa Somalia hadi kufikia bandari yao inayofuata.

Jukumu rasmi la manuwari hiyo, ilio na mabaharia 240, mnamo wiki nne zijazo, ni kufanya uchunguzi katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Kazi ya manwari hiyo ni kupiga doria katika mwambao wa Mashariki ya Afrika. Kwa hakika mapambano hayo kwa muda sasa yamegeuka kuwa ni dhidi ya maharamia; hivyo, kuna uwezekano wa kutokea hatari za ziyada.

Nahodha Schönbach anasema hali ya usalama imebadilika hasa mnamo wiki moja au mbili zilizopita. Alisema wao wanajuwa kwamba hata meli za nchi za muungano wa kupambana na ugaidi zinaweza kushambuliwa. Na vipi hali hiyo itakavokuwa, itawabidi waangalie. Kwa vyovyote inawabidi wawe waangalifu zaidi.

Nahodha huyo alisema wanaendelea kufanya mazoezi ya kutunga shabaha za kufyetua risasi na silaha zao zote ziko katika hali ya tayari tayari. Hapo kabla walikuwa wanazishughulikia aina fulani za boti, lakini sasa lazima wachukulie kwamba kitisho kinaweza kikatokea kutoka upande wowote.Pia mabaharia wameambiwa watume barua za noeli hadi Disemba 4, japokuwa inajulikana kwamba jamaa wa mabaharia hao hapa Ujerumani wanangojea kwa hamu zaidi kuliko miaka iliopita kujuwa kama mambo yote ni salama ndani ya manuwari hiyo.

Rebecca Broksch, daktari a meno katika manuwari hiyo anasema hivi:

"Mimi binafsi nahisi yeyote yule anayesema kwamba anaweza kujisahaulisha na hali hii, kwamba anasafiri kama vile yuko katika Bahari ya Mashariki , kaskazini mwa Ulaya, anapokuwa katika mazoezi, mimi mtu akisema hivyo si amini kabisa. Bila ya shaka mtu ana wasiwasi. Na jambo hilo mtu anahisi pale mtu anapokuwemo katika shughuli za kila siku."

Ndani ya manuwari hiyo kunafanwa mazowezi ya kuwaokoa watu wanapojuruhiwa, kuna daktari wa upasuaji na yule anyeshughulikia nusukaputi. Pindi kunatokea mapigano, kepteni wa manuwari Thomas Stötzel anayeusimamia mtambo wa Rader hupokea risala kutoka makao makuu ya jeshi la muungano la kupambana na ugaidi huko Bahrein. Yeye kila wakati hungojea maagizo yalio wazi kutoka Berlin pindi kunatokea mkaasa wowote.

"Mtu hajuwi nini kitakachotokea, bahati mbaya ni kwamba katika siasa za Ujerumani mambo sio yalivyo kwamba serekali huamuwa kwa haraka, lakini kwanza kutazungumzwa na kuzungumzwa. Na hapa mtu anajikuta peke yake. Mtu anangoja kwamba uamuzi ufikiwe, na kila siku mtu anakabiliana kutoka kwa wanasiasa na vyombo vya habari na shuku hizi na zile. Ingekuwa rahisi mtu aweze kupata tamko wazi kutoka serekalini au kutoka kwa wanasiasa, ili mtu aweze kuambiwa kwamba hiki tunaruhusiwa na kile haturuhusiwi kufanya."

Mada hii itazungumuiwa bungeni mjini Berlin hapo Disemba 3, kwani wachunguzi wa mambo wanahofia kutokuweko mchafuko pale manuwari za mataifa mbali mbali zikiwa na majukumu tafauti zitakapokuwa zinafanya operesheni za kuwaandama maharamia, kwani Warussia, Wahindi, ambao hawamo katika jumuiya ya NATO, watakuwa pia wanazisindikiza meli zao za biashara katika eneo hilo la Guba ya Yemen.

Vyama vya upinzani hapa Ujerumani zimeielezea operesheni za manuwari zao kuwa ni kichekesho kwa vile mabahria wa Kijerumani, kwa mujibu wa katiba ya nchi, hawatakiwi kuwakamata maharamia hao, na ukitokea mkasa basi lazima wamsafirishe muendeshaji mashtaka kutokea Hamburg awafungulie mashtaka hao wanaotuhumiwa kuwa maharamia.
 • Tarehe 28.11.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G5Sy
 • Tarehe 28.11.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G5Sy
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com