Operesheni yaanzishwa kuukomboa mji wa Kunduz | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Operesheni yaanzishwa kuukomboa mji wa Kunduz

Majeshi ya Afghanistan yakisaidiwa na ndege za kivita za Marekani, yameanzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Kunduz, siku moja baada ya wapiganaji wa Taliban kuudhibiti mji huo ulioko kaskazini mwa Afghanistan.

Vikosi maalum vya Afghanistan

Vikosi maalum vya Afghanistan

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Kanali Brian Tribus, imeeleza kuwa majeshi ya Marekani yamefanya mashambulizi ya anga kwenye mji wa Kunduz kwa lengo la kuwafurumusha wanamgambo wa kundi la Taliban. Kanali Tribus amesema mashambulizi hayo ya anga yaliyoanza mapema leo asubuhi yamefanyika katika kupambana na kitisho dhidi ya vikosi vya Afghanistan pamoja na vile vya muungano vinavyoongozwa na NATO

Kitendo cha Taliban kuudhibiti mji huo ni ushindi mkubwa kwa kundi hilo tangu lilipoondolewa madarakani mwaka 2001. Wanamgambo wa Taliban jana walifanya mashambulizi makubwa katika makao makuu ya mji wa Kunduz na kuyadhibiti majengo muhimu ya serikali na kuwaachia huru mamia ya wafungwa ambao ni wanachama wake, wakiwemo makamanda wa Taliban pamoja na kupeperusha bendera nyeupe kuuzunguka mji huo wakionyesha alama ya ushindi.

Akizungumza baada ya Taliban kufanya mashambulizi na kuudhibiti mji wa Kunduz, Kamanda wa vikosi vya ardhini na naibu mkuu wa majeshi wa Afghanistan, Jenerali Murad Ali Murad, amesema mashambulizi hayo ni kitendo cha kigaidi kilichofanywa na makundi kadhaa.

Wanamgambo wa Taliban

Wanamgambo wa Taliban

''Shambulizi lilifanywa na makundi tofauti ya kigaidi ya ndani na yale ya kigeni, huku yakiungwa mkono na mitandao ya kigaidi ya kigeni. Washukuru kutokana na msaada huo wa kigeni, yalifanikiwa kuingia kwenye mji wa Kunduz na kuudhibiti,'' alisema Murad.

Kunduz kukombolewa

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afghanistan, Ayoub Salangi, awali alisema vikosi vya usalama viko tayari kuukomboa na kuutwaa tena mji wa Kunduz na ameahidi kufanya uchunguzi wa kubaini ni kwa namna gani wanamgambo wa Taliban waliweza kuudhibiti mji huo muhimu kwa mara ya kwanza tangu miaka 14 iliyopita.

Wizara ya ulinzi ya Afghanistan leo imedai kuwa makao makuu ya polisi pamoja na gereza lililoko mjini, yamekombolewa na vikosi vya usalama. Hata hivyo, baadhi ya majengo ya serikali, ikiwemo hospitali yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 200 bado yako mikononi mwa Taliban.

Rais Ashraf Ghani

Rais Ashraf Ghani

Kwa mujibu wa wizara hiyo, vikosi vya serikali vilivyoweka kambi usiku kucha kwenye uwanja wa ndege wa Kunduz, vitaukomboa hivi karibuni mji huo. Wizara hiyo imesema wanajeshi wapya waliwasili kwenye mji wa Kunduz na operesheni imeanzishwa.

Kitendo cha mji wa Kunduz kuangukia ghafla mikononi mwa Taliban ni pigo kubwa kwa serikali ya Rais Ashraf Ghani, ambayo Jumanne ya leo imetimiza mwaka mmoja madarakani, hivyo kuzusha maswali mengi iwapo vikosi vya Afghanistan kweli viko tayari kupambana na kundi la Taliban, vyenyewe bila ya usaidizi wowote.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,RTRE
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com