1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni Sophia kusitishwa bahari ya Mediterania

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssesanga
27 Machi 2019

Operesheni hiyo ilikuwa ya kupambana na wafanyabiashara haramu ya kuwasafirisha wahamiaji katika bahari ya Mediterania na wakati huo huo kuwaokowa watu waliokabiliwa na hatari kwenye bahari hiyo.

https://p.dw.com/p/3FhmA
Libyen Migranten auf Marine-Boot
Picha: Reuters/I. Zitouny

Hatua hiyo inatokana na uamuzi unaolenga kutatua mgogoro kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na mwanachama mwenza Italia juu ya mahala pa kuwahifadhi watu pindi wanapookolewa.

Vyanzo vya Umoja wa Ulaya vimesema meli zilizokuwa zinatumika kwenye mpango huo hazitakuwa tena sehemu ya Umoja wa Ulaya katika operesheni Sophia kuanzia mwezi ujao. Italia ilikuwa imetishia kuusitisha mpango huo isipokuwa kwa masharti kwamba wahamiaji waliookolewa wangepelekwa katika nchi nyingine pia.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, mazungumzo yaliyofanyika siku ya Jumanne mjini Brussels yalifikia makubaliano kwamba uendeshaji wa shughuli za uokozi utatekelezwa kwa muda wa miezi mingine sita bila ya meli hizo mbili kuwepo baharini lakini hatua ya kuimarisha  doria itafanyika kwa njia ya anga. Wakati huohuo mafunzo yanayotolewa kwa walinzi wa pwani wa Libya yataendelea chini ya mipango inayoendelea. Iwapo hakutakuwepo na pinganizi lolote, mpango mpya uliofanyiwa marekebisho utaanza kufanya kazi kuanzia Aprili Mosi.Operesheni Sophia iliongezewa muda mfupi wa miezi mitatu mnamo mwezi Desemba mwaka jana baada ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kushindwa hawakukubaliana juu ya hatua za muda mrefu.

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo SalviniPicha: picture-alliance/NurPhoto/P. Manzo

Italia wakati wote imekuwa inaipinga sera ya kuwapokea moja kwa moja wahamiaji waliokolewa na ambao kimsingi walipelekwa katika bandari za Italia na mara kwa mara ilitoa vitisho kwamba itawasilisha kesi mahakamani kuzuia mpango huo wa uokoaji kama sheria za ushiriki hazibadilishwa. Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini amesema nchi yake haiwezi kuubeba mzigo wa wakimbizi peke yake.  

Nchi nyingine wanachama zimekuwa zinakataa kuwachukua wahamiaji kwa madai kwamba hawakufikia kwanza kwenye nchi yoyote ya Umoja wa Ulaya kupitia kwenye mipaka ya nchi husika.

Tangu operesheni Sophia ilipoanza mnamo mwaka 2015, zaidi ya watu 45,000 wameokoloewa kutoka baharini. Lengo lake lilikuwa kupambana na makundi ya wafanyabiashara haramu kutoka Libya, lakini pia inahusika na kuiwekea Libya vikwazo vya silaha. Nchi hiyo imo kwenye mgogoro unaoendelea tangu kuanguka kwa utawala Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, amewalaumu makamanda wa Italia kwa kusema wamekuwa wakiziegesha meli zao mbali zaidi na sehemu ambazo zilikuwa zinatumiwa kama njia za kuwasafirisha wakimbizi.

Ni meli mbili pekee zilizotumiwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita baada ya Ujerumani kuiondoa Manowari yake ya kijeshi "Augsburg" mwezi Januari.

Vanyo Zainab Aziz/p.dw.com/p/3FhYE