1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la bei za chakula lajadiliwa na viongozi wakuu duniani

Mwakideu, Alex29 Aprili 2008

Umoja wa Mataifa umetenga jopo maalum litakaloshughulika na tatizo kuongezeka kwa bei za vyakula

https://p.dw.com/p/Dqr5
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alipokuwa akifungua mkutano unaohusu biashara na maendeleo mjini Accra GhanaPicha: AP

Umoja wa Mataifa utatenga jopo maalum kitakachoongozwa na katibu mkuu wa Umoja huo Ban Ki Moon. Kikosi hicho kinaundwa kwa nia ya kukabiliana na ongezeko la bei za vyakula duniani.


Viongozi wa Umoja wa Mataifa wameamua kuchukua hatua kadhaa ili waweze kupata suluhisho la dharura na pia siku za usoni.


Jambo ambalo litapewa kipau mbele zaidi ni ongezeko la dola laki saba na hamsini na tano zinazohitajika na shirika la chakula duniani ili kuwasaidia mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa kutokana na ongezeko la bei za vyakula.


Ban amesema lazima kuwe na uhakika wa kupatikana kwa chakula katika siku za mbeleni.


Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa lina mpango wa kutumia dola bilioni 1.7 kugawa mbegu kwa wakulima wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani.


Ban ameongezea kwamba mikakati mipya ya Umoja wa Mataifa inapaswa kuzingatia maswala nyeti zaidi badala ya kugawa chakula cha msaada wakati wa shida.


Umoja wa Mataifa umegundua kwamba tatizo la ongezeko la bei ya chakula limefikia hali ambapo haliathiri maskini wa mashambani pekee bali hata wale wanaoishi mijini.


Ongezeko la bei ya chakula limezua njaa, maandamano na ghasia katika nchi kadhaa maskini.


Bei ya juu kwa ngano, mchele, na vyakula vingine vya kila siku imekuwa tatizo kubwa kwa shirika la chakula duniani linalolenga kuwalisha watu milioni 73 mwaka huu.


Katika taarifa yake Rais wa benki ya dunia Robert Zoellick amesema Benki ya dunia itafanya kazi na Umoja wa Mataifa kuzikagua nchi zinazohitaji misaada zaidi ili kwa pamoja tuweze kutoa misaada ya kifedha na mingineo. Katika benki ya dunia tunafikiria kutenga mfuko wa dharura utakaosaidia nchi maskini na pia kurahisisha maisha kwa nchi nyinginezo.


Mwaka ujao Benki hiyo itaongeza mara dufu msaada wake kwa ukulima barani Africa ili ufikie dola milioni mia nane.


Zoellick na katibu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon wametoa wito kwa nchi zote duniani zisipige marufuku usafirishaji wa chakula wakisema kwamba hatua hiyo inazidisha tatizo la chakula duniani.


Zoellick amesema kando na hatua za dharura jamii ya kimataifa sharti itafute utatuzi wa ongezeko la bei ya chakula kwa siku za usoni kama kuimarisha biashara ulimwengu mzima.


Mkuu wa shirika la biashara duniani Pascal Lamy amesema tatizo la ongezeko la bei za vyakula ni sababu nzuri ya kumaliza mazungumzo ya biashara ya Doha na kufungua biashara ya dunia.


Mazungumzo hayo yaliyoanzishwa mwaka wa 2001 yameimarisha biashara ya chakula na bidhaa zingine kwa kukata kodi.

Lamy amesema ana imani kwamba tatizo la chakula litawafanya wanachama wa shirika la biashara duniani kupata motisha ya kusaidia nchi zinazokua kuongeza mazao ya chakula.