1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ombi la Kabendera la kumzika mamake latupiliwa mbali

Amina Mjahid
2 Januari 2020

Kesi inayomakabili mwandishi wa habairi Eric Kabendera nchini Tanzania imehairishwa tena hadi Januari 13, huku ombi la mwandishi huyo kutaka kushiriki kumuaga mama yake aliyefariki dunia likikataliwa na mahakama.

https://p.dw.com/p/3VcIV
Tansania Erick Kabendera vor Gericht
Picha: DW/S. Khamis

Mwandishi alipanda kizimbani nyakati za asubuhi akiiomba mahakama hiyo imruhusu kuungana na ndugu na jamaa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mama yake mzazi Verdiana Mjahuzi aliyefariki dunia Disemba 31 akiwa na umri wa miaka 80.

Mahakama imekataa kumkubalia ombi lake na kwa maana hiyo ataendelea kusalia rumande wakati mwili wa mama yake uikiagwa na kusafirishwa hadi huko Bukoba atakakozikwa Januari 6.

Mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi lililotolewa na mawakili wa Jamhuri waliosema kwamba kimsimgi mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa idhini kwa mshtakiwa huyo kwenda kushiriki shughuli za mazishi.

Uamuzi huo wa mahakama ulipokelewa kwa hisia za majonzi kutoka kwa familia ya mwandishi huyo wa habari kiasi cha baadhi kungua kilio.

Siku za mwisho mwisho wa uhai wake, mama yake Kabendera aligonga vichwa vya habari pale alipomwomba Rais John Magufuli amsamehe mwanaye kwa vile alikuwa tegemeo lake kubwa wa kumsaidia katika kupata huduma za matibabu.

Kesi ya Kabendera itasikilizwa tena Januari 13

Tansania Erick Kabendera vor Gericht
Picha: DW/S. Khamis

Eric Kabendera alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwaka uliopita akikabiliwa na mashataka matatu ikiwamo utakatishaji wa fedha wa shilingi milioni 173 na kushiriki katika genge la uhalifu. Shtaka lingine ambayo yote kwa pamoja hayana dhamana ni kukwepa kulipa kodi ya shilingi milioni 73.

Mawakili wake wamekuwa wakiyakana makosa hayo na wakati fulani walisema kesi dhidi ya mteja wao inahusishwa na kazi yake ya uandishi wa habari.

Mbali ya kufanya kazi katika vyombo vya habari vya nchini, Eric Kabendera amekuwa akifanya kazi na vyombo vya habari vya nchi za magharibi na amekuwa akichambua masuala mengi yanayohusu siasa na uchumi.

Kesi yake leo ilishindwa kuendelea katika mahakama ya kisutu baada ya upande wa Jamhuri kudai upepelezi bado haujakamilika. Anatarajiwa kurejea tena mahakamani hapo Januari 13.

Mwandishi: George Njogopa