1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert yuko tayari kukutana na viongozi wa Kiarabu.

Mohamed Dahman15 Mei 2007

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema leo hii kwamba yuko tayari kukutana na viongozi wa Kiarabu kujadili mpango wao wa amani lakini bila ya kuwekewa masharti.Kauli yake hiyo inakuja wakati Umoja wa Waarabu ukitowa wito wa kusitishwa kwa utanuzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi na huku kukiwa na mapigano kati ya makundi hasimu ya Kipalestina ya Fatah na Hamas.

https://p.dw.com/p/CHEJ
Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.
Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.Picha: AP

Olmert akiwa nchini Jordan amekaririwa akisema kwamba anawaalika viongozi hao 22 wa mataifa ya Kiarabu ambao wako tayari kuwa na amani na Israel kwenda wakati wowote wanaotaka kukaa kitako na Israel na kuanza kuzungumza na kuwasilisha mawazo yao.

Amewaambia washindi wa tuzo ya amani ya Nobel waliokusanyika katika mji wa Petra kabla ya mazungumzo yake na Mfalme Abdaullah wa Jordan kwamba likiwa jambo hilo ni gumu kwao yeye yuko tayari kwenda popote pale kukutana nao.

Amesema wako tayari kukaa chini na kuwasikiliza kwa makini na kwamba bila ya shaka watakuwa na ya kusema juu ya mpango huo ambapo watabadilishana mawazo.

Mpango huo uliopitishwa hapo mwezi wa Machi katika mkutano wa viongozi wa Waarabu unapendekeza kurudisha uhusiano kamili na Israel ili nayo nchi hiyo iondoke kutoka ardhi ya Waarabu ilioiteka mwaka 1967,kuundwa kwa taifa la Palestina na kurudishwa kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Awali Israel iliukataa mpango huo wakati ulipowasilishwa kwa mara ya kwanza hapo mwaka 2002 na Saudi Arabia lakini baadae Olmert amekaribisha kwa hadhari baadhi ya vipengele vya mpango huo juu ya kwamba Israel inataka kufanywe marekebisho katika suala la wakimbizi.

Israel pia inasisitiza kwamba mazungumzo na mataifa ya Kiarabu yafanyike sambamba na mazungumzo ya amani ya pande mbili kati ya Israel na Wapalestina ambayo yamekwama tokea mwaka 2001.

Umoja wa Waarabu leo hii umeitaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Israel kusitisha mipango yake kwa utanuzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Jerusalem ya Mashariki ya Waarabu inayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Umoja huo wa nchi wanaachama 22 hususan umelitaka kundi la pande nne juu ya amani ya Mashariki ya Kati linaloundwa na Umoja wa Mataifa,Marekani,Umoja wa Ulaya na Urusi kuwajibika na kukomesha uhalifu huo mpya wa Israel.

Mpango huo unaotazamia ujenzi wa zaidi ya nyumba 20,000 umeandaliwa na kamati ya manispaa na lazima uidhinishwe na mamlaka za taifa.

Wapalestina wameazimia kuufanya Jerusalem ya Mashariki kuwa mji mkuu wao wa baadae na umoja wa Waarabu unaishutumu Israel kwa kuendeleza utanuzi huo ili kukwepa mazungumzo juu ya hatima ya mji huo.

Wakati huo huo Wapalestina 10 wameuwawa katika mapambano kati ya makundi hasimu ya Kipalestina ya Fatah na Hamas katika Ukanda wa Gaza leo hii.

Askari wanane wa kikosi cha rais wameuwawa katika Ukanda wa Gaza ya kaskazini kwa kile vikosi vya usalama vilivyo tiifu kwa kundi la Fatah la Rais Mahamoud Abbas walichosema ni shambulio la Hamas kwa kambi ya mafunzo.

Msemaji wa serikali ya Palestina Ghasi Hamad amethibitisha kwamba wamefikia makubaliano katika mikutano kati ya Waziri Mkuu Ismael Haniyeh na viongozi wa Hamas na Fatah ambayo yalipaswa kuanza kutekelezwa hapo jana usiku.

Amesema wanza kabisa rais anatowa amri kwa vikosi vyote vya usalama kuondoka mitaani na anafikiri kwamba makundi ya Hamas na Fatah yameagiza wafuasi wao walioko mitaani kuondoka na kusitisha mizozo na mapambano yote ya kijeshi mitaani na kuwarudisha wale wote waliotekwa nyara na pia kukomesha uchochezi kwenye vyombo vya habari.

Wapalestina 18 wameuwawa hadi sasa tokea kuzuka kwa mapigano kati ya Hamas na Fatah hapo Jumapili na zaidi ya 50 wamejeruhiwa na kutowa pigo kubwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kukomesha mfarakano huo ikiwa ni miezi miwili tu tokea iingie madarakani.