Oliver Kahn atachukua nafasi ya Rummenigge Bayern Munich
30 Agosti 2019Mabingwa hao mara nyingi nchini Ujerumani wamesema siku ya Ijumaa (30.08.2019) kwamba Kahn mwenye umri wa miaka 50 , nahodha wa zamani wa bayern na mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani, amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo utakaoanza Januari 1, 2020, baada ya kuthibitishwa katika mkutano wa bodi ya utendaji siku ya Alhamis.
Kahn ambaye hivi sasa anafanyakazi kama mfanyabiashara na mtaalamu wa televisheni katika michezo, amekuwa akifikiriwa kwa kiasi kikubwa kuchukua nafasi ya Rummenigge mwenye umri wa miaka 63, ambaye atajiuzulu wakati mkataba wake utakapofika mwisho Desemba 31, 2021.
"Ni heshima kubwa kwangu kwamba nitaaminiwa kushika wadhifa katika ofisi kama mwanachama wa bodi ya bayern Munich na baadaye katika ofisi ya mtendaji mkuu CEO na mwenyekiti wa bodi ya utendaji ya Bayern Munich," Kahn alisema katika taarifa.
Kahn mteule wa Hoeness
"Ningependa kuishukuru bodi ya uangalizi , ikiongozwa na Uli Hoeness, kwa kuniamini."
Kahn alikuwa mteule aliyependelewa na Hoeness, ambaye binafsi anajitayarisha kujiuzulu kutoka katika medani kuu ya Bayern Munich.
Siku ya Alhamis rais aliyeitumikia klabu hiyo kwa muda mrefu alisema hataomba kuchaguliwa tena hapo Novemba 15.
"Nina mahusiano ya karibu na klabu hii na imejenga maisha yangu," Kahn amesema. "Mafanikio ya kimichezo na kifedha, mshikamano na mashabiki, uendeshaji wenye kuwajibika kuelekea katika historia ya klabu hiyo na maadili, hivi ndivyo Bayern inavyovisimamia."
Kahn alianza kucheza kandanda akiwa na klabu ya karlsruhe kbla ya kuhamia Bayern Munich mwaka 1994 na kumtengeneza kuwa mlinda mlango nyota.