1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpik na siasa

1 Agosti 2008

Rais Hu Jintao wa China, ametaka siasa itengwe nje ya michezo ya olimpik.

https://p.dw.com/p/EoQP

Tangu mwenge wa olimpik kupita katika miji ya magharibi ukiwa njiani kuelekea Beijing,kwa ufunguzi wa michezo ya 29 ya olimpik ijumaa ijayo ,siasa zimekuwa zikiandamana na michezo ya Beijing , 2008.China imetuhumiwa kuvunja ahadi ilizotoa ilipotunukiwa nafasi ya kuiandaa michezo hii. Ikiweka vikwazo vya habari katika mtandao wa Internet ambavyo sasa imeviondoa. Ikaahidi pia kukuza haki za binadamu.

Ijumaa ijayo,marais na viongozi wa serikali kiasi cha 80 pamoja nao George Bush wa Marekani, watahudhuria ufunguzi rasmi katika uwanja mkuu wa kisasa kabisa wa Beijing.Machafuko ya Tibet yaliozimwa kwa mkono wa chuma na vikosi vya usalama vya China na ukaguzi uliofuatia wa habari kutoka Beijing kupitiab mtandao wa Internet, kumeengeza kama inavyotokea mara kwa mara, mchezo 1 zaidi katika kalenda ya olimpik 2008-mchezo wa siasana Olimpik.

Rais wa China Hu Jintao, alitoa mwito ijumaa kuweka kando siasa na olimpik.

Je, itawezekana ? Mara nyingi michezo ya olimpik imekuwa ikiandamwa na siasa: Ilikua hivyo, Mexico City, 1968, Munich 1972 na Montreal ,1976 ilipotishiwa kugomewa na wanariadha wa Afrika.Na halkadhalika, tulijionea Marekani na washirika wake wakiigomea michezo ya Moscow, 1980 baada ya Urusi kuivamia Afghanistan. Urusi na washirika wake nao wakaisusia michezo ya 1984 ya Los Angeles.

Haikusangaza kwahivyo, kumsikia jana Rais wa China Hu Jintao, kutoa mwito kutenga siasa nje ya Olimpik.Akijribu hapo kuzima ila kali zilizotolewa

ulimwenguni wiki kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo ilioianika hadharani vipi china inavyoendesha mambo ndani na nje.

Baadhi ya mawasiliano ya Internet yalizimwa ,lakini kufuatia malalamiko makali yalirejeshwa hapo ijumaa .Hatahivyo, rais wa China Hu jintao, alionya kwamba ni kinyume na moyo wa olimpik kuchanganyisha siasa na michezo na kulketa maswali kama hayo ya kisiasa usoni mwa mji wa Beijing hakusaidii kitu.

Michezo ya Beijing inatumainiwa na wenyeji China, kuonesha nguvu zake zinazoongezeka ulimwenguni kama dola kuu. Kiasi cha waandishi habari 20,000 wa Radio,TV na magazeti wamo kuwasili Beijing na uongozi wa chama kikuu cha kikominist cha China unajikuta unachunguzwa barabara kuliko wakati wowote kabla tena kutoka ndani ,kwani imewafungulia mlango waandishi hao.China imejaribu sana kuwalazimisha kushughulikia spoti tu na sio siasa na haki za binadamu, bila ya mafanikio.

Kuanzia mkomoto huko Tibet hadi malalamiko yalioandamana na mwenge wa olimpik,usuhuba wake na Sudan, inayolaumiwa kukanyaga haki za binadamu mkoani Dafur, siasa imekua ikitokeza kichwa chake mara kwa mara katika michezo hii.

Hatua ya China kuzima mawasiliano ya mtandao wa Internet yaliifedhehesha mno Halmashauri Kuu ya Olimpik Ulimwenguni (IOC).

Rais wa IOC Jacques Rogge mwezi uliopita aliahidi kwamba vyombo vya habari vya kigeni vingepewa uhuru kamili katika Internet.

Kufuatia malalamiko, jana mtandao wa shirika linalotetea haki za binadamu ulimwenguni-Amnesty International, shirika la maripota wasio na mipaka na hata kituo hiki Deutsche Welle yameondolewa vizuwizi hivyo.

Njia sasa yaonesha iko wazi kwa ufunguzi ijumaa ijayo,lakini tusitumai tu kuwa risasi za mwisho katika vita kati ya siasa na Olimpik zimefyatuliwa.

Hii inatukumbusha onyo kali la rais wa zamani wa IOC-Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni, marehemu Avery Brundage: yeye alisema:

"Zamani huko Olympia wakati wa Olimpik, ugomvi wote ukiwekwa kando ili kushiriki katika Olimpik, leo watu wanaweka kando olimpik kwenda vitani."