1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga apinga matokeo ya uchaguzi Mahakama ya Juu

16 Machi 2013

Mgombea wa urais alieshindwa katika uchaguzi Kenya Raila Odinga Jumamosi(16.03.2013) amewasilisha pingamizi ya kisheria mahkamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo ukiwa ni mtihani mkubwa kwa demokrasi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/17z0U
Waziri Mkuu Raila Odinga
Waziri Mkuu Raila Odinga.Picha: Reuters

Polisi waliokuwepo nje ya Mahakama Kuu walitumia gesi ya kutowa machozi kuwatawanya wafuasi takriban 100 wa Odinga ambao walitakiwa na waziri mkuu huyo anayeondoka madarakani kuwa watulivu na waiamini sheria katika kuyapatia ufumbuzi malalamiko yao. Hatua hiyo ya Odinga inatishia kurefusha kipindi cha wasi wasi chenye kuligubika taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi Afrika Mashariki.

Odinga anagoma kuutambua ushindi mdogo wa Uhuru Kenyatta alioupata katika duru ya kwanza ya uchaguzi.Kenyatta anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ya ICC kutokana na ghasia za mwaka 2007 ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuwawa.

Uchaguzi huu wa tarehe 4 Machi kwa kiasi kikubwa ulifanyika kwa amani tafauti kabisa na ule wa mwaka 2007  ambapo Kenyatta katika hotuba yake ya kukubali matokeo wiki iliyopita amesema ulikuwa huru na wa haki juu ya kwamba ameongeza kusema kwamba mchakato huo wa uchaguzi unaweza kuboreshwa zaidi na kuwa wa ufanisi katika kipindi kijacho.

Sababu za Odinga kugomea matokeo

Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) iliahidi uchaguzi huo ungelifanyika kwa utulivu lakini kusambaratika kwa mfumo mpya wa kupiga kura kwa njia ya elektroniki wenye gharama kubwa kumesababisha watu wasubiri kwa siku tano kutangazwa kwa mshindi.

Polisi wa kutuliza ghasia wakiwatimua wafuasi wa Odinga nje ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi (16.03.2013)
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwatimua wafuasi wa Odinga nje ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi (16.03.2013)Picha: Reuters

Pingamizi hilo la Odinga la kupinga matokeo ya uchaguzi linadai kuwepo kwa udanganyifu mkubwa na kuituhumu tume ya IEBC kwa kuongeza idadi ya usajili wa wapiga kura na kuendelea kufanya uchaguzi huo licha ya kutambuwa kwamba mifumo yake itakuja kushindwa kufanya kazi.

Odinga amewaambia waandishi wa habari akiwa nje ya ofisi yake katikati ya mji mkuu wa Nairobi kwamba kushindwa kufanya kazi kwa mifumo hiyo kumedumaza kila kitu ambacho Wakenya hawakuwahi kamwe kushuhudia katika chaguzi zozote zile zilizopita.

Amesema kila utaratibu na kila zana iliyotumiwa na tume ya uchaguzi ya Kenya vimeshindwa vibaya sana na kwamba kushindwa na kusambaratika kwake huko kwa kiwango kikubwa wakati wa siku ya uchaguzi kumebadili kabisa mfumo wa kupiga kura na idadi ya kura zilizopigwa.

Ushindi wa Kenyatta

Kenyatta alipata ushindi wa haja dhidi ya Odinga kwa kuzingatia kura alizopata asilimia 50.07 ya kura dhidi ya asilimia 43.28 lakini ameepuka chupuchupu marudio ya uchaguzi baada ya kushinda kura 8,100 zaidi ya asilimia hamsini inazohitajika kuweza kutangazwa moja kwa moja kama mshindi.

Rais Mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta na mke wake Margaret.
Rais Mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta na mke wake Margaret.Picha: REUTERS

Hali hiyo ya ushindi usio mkubwa wa Kenyatta imewapa washirika wa Odinga imani kwamba wanaweza kupitia mahakama kulazimisha kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa pingamizi yao ya kisheria yenye kutaka mchakato huo mzima utangazwe kuwa batili na haufai.

Wakati pingamizi hilo lilipowasilishwa mapema hapo mchana mamia ya wafuasi wa Odinga walikuwa wamekusanyika nje ya mahakama wengi wao wakiwa wamevalia fulana zenye kauli mbiu kama vile "demokrasia iko kwenye mtihani". Magari yalikuwa yakitembea bila ya mtatizo katika mji mkuu wote wa Nairobi na kulikuwa hakuna ishara ya machafuko zaidi katika mji huo.

Hofu ya marudio ya ghasia

Wengi walikuwa wakihofu marudio ya ghasia za mwaka 2007  baada ya uchaguzi wa mwezi huu na walifarajika wakati jambo halikutokea. Lakini wachambuzi wanasema ufumbuzi wa haraka na ulio wazi kwa mzozo huo ni muhimu kurejesha sifa ya Kenya kama taifa imara la demokrasia.

Wanajeshi wa kutuliza ghasia wakiwa katika doria nje ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi (16.03.2013).
Wanajeshi wa kutuliza ghasia wakiwa katika doria nje ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi (16.03.2013).Picha: Reuters

Wafadhili wakuu wa mataifa ya magharibi wana wasi wasi na taifa hilo ambalo ni mshirika muhimu katika mapambano ya kupiga vita harakati za wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu katika kanda hiyo.

Pingamizi hiyo ya kisheria ya Odinga inailalamikia IECB, mwenyekiti wa tume hiyo Isaack Hassan, Kenyatta na mgombea wake mwenza William Ruto ambaye pia anashtakiwa na mahakama ya ICC kwa  uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na ghasia za baaada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Uamuzi wa Odinga kupinga matokeo hayo ya uchaguzi mahakamani ni tafauti na ule aliouchukuwa mwaka 2007 kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo pia aliyaelezea kuwa yalichakachuliwa.Odinga wakati huo aliwataka wafuasi wake watoke barabarani kwa maandamano ya amani kutokana na kutoiamini mahakama kuwa itatenda haki. Lakini ghasia ziliripuka kwa ghafla kati ya makabila yenye kuunga mkono wagombea wanaowania uongozi na kuenea nchini kote Kenya.

Mwandishi: Mohamed Dahman/REUTERS
Mhariri: Iddi Ssessanga