1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kutangaza sheria za kudhibiti gesi chafu

3 Agosti 2015

Rais wa Marekani Barack Obama atazindua leo kile anachokiita “hatua kubwa kabisa na muhimu kuwahi kuchukuliwa” katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/1G8pM
Obama unterschreibt Executive Order
Picha: picture-alliance/dpa/Sachs

Rais huyo amesema kuzuia kuongezeka kwa joto duniani ni miongoni mwa masuala muhimu katika utawala wake.

Rais Obama alionesha nia yake kwa kutoa ujumbe kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii Facebook hapo jana, akisema sheria hizo mpya zitalenga kupunguza gesi chafu kutoka katika viwanda vinavyotumia makaa ya mawe. "Hali ya hewa inabadilika. Inabadilika katika njia ambayo inahatarisha uchumi wetu, usalama wetu na afya yetu. Haya sio maoni. Ni ukweli unaotokana na miongo mingi ya data zilizokusanywa na utafiti wa kisayansi. Hali hii inaathiri namna tunavyoishi".

Sheria hizo zimekuwa zikifanyiwa kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Wakati zilipopendekezwa mwaka jana, utawala wa Obama ulidokeza kuwa gesi ya kaboni inayotoka katika viwanda vya umeme itahitaji kupunguzwa kwa asilimia 30 chini ya viwango vya mwaka wa 2005 ifikapo mwaka wa 2030. Lakini sheria za mwisho itahitaji kupunguzwa kwa asilimia 32.

Demonstration für Klimaschutz in Washington
Wanaharakati wa mazingira wakiunga mkono sheria za kupunguza gesi ya kaboniPicha: Reuters

''Mabadiliko ya tabia nchi sio tatizo la kizazi kinachofuata'', Amesema Obama, na kuongeza kuwa ''Hatuwezi kuwaweka watoto wetu na wajukuu katika sayari isiyoweza kurekebishwa''.

Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi ni suala la msingi katika malengo ya urais wa Obama. Huku mazungumzo muhimu ya kimataifa yakisubiriwa Desemba mjini Paris, Obama amepiga hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuiweka Marekani kwenye mkondo safi na kuishawishi China, nchi inayoongoza ulimwenguni katika uzalishaji wa gesi chafu kufuata mkondo huo.

Marekani ndiyo nchi ya pili duniani inayozalisha gesi ya kaboni. Obama amesisitiza kitisho kinachoongezeka kuanzia ukame, mafuriko, vimbunga vikubwa wakati joto likiendelea kuongezeka duniani kutokana na uzalishaji wa gesi chafu ambayo hunasa joto angani.

Mpango wa Obama wa Umeme Safi utayahitaji majimbo yote ya Marekani kuchukua hatua ya kudhibiti uzalishaji wa gesi ya kaboni. Magavana wa Republican wameanzisha kampeni ya kuwasilisha suala hilo mahakamani wakiongozwa na magavana wa majimbo yanayozalisha makaa ya mawe ambayo yanapinga mamlaka ya Obama ya kudhibiti uzalishaji wa gesi ya kaboni. Kesi hiyo huenda ikafikishwa katika Mahakama ya Juu.

Kiongozi wa upande wa upinzani katika baraza la Seneti, Mrepublican anayetoka katika jimbo la Kentucky linalozalisha kiasi kikubwa cha makaa ya mawe, alisema mwaka jana kuwa Obama ameanzisha vita dhidi ya makaa ya mawe. Chama hicho cha kihafidhina kinapuuza kwa kiasi kikubwa wasiwasi kuhusu ongezeko la joto duniani na ushahidi wa kisanyansi ambao unaashiria mabadiliko ya tabia nchi.

Kuzinduliwa kwa mpango huo wa mwisho kunafuatia juhudi ambazo hazikufaulu za Obama kulishawishi Bunge la Marekani kupitisha sheria inayosimamia udhibiti wa gesi ya kaboni. Mnamo mwaka wa 2013, Obama aliruhusu miradi ya nishati mbadala kama vile inayotumia jua na upepo. Jeshi la Marekani limeorodhesha mabadiliko ya tabia nchi kuwa kitisho kwa usalama wa taifa.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Daniel Gakuba