Obama kuongeza wanajeshi Afghanistan | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Obama kuongeza wanajeshi Afghanistan

Marekani itatuma vikosi vya wanajeshi, wengine 4,000 nchini Afghanistan kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo, chini ya ule mkakati mpya wa Rais Barack Obama kupambana na waasi wa Kitaliban.

Rais Barack Obama

Rais Barack Obama


Na mjini Moscow katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa wale wanaohudhuria mkutano wa kimataifa kuzungumzia ulanguzi wa dawa za kulevya na usalama Afghanistan. Haya yanafanyika siku nne tu kabla mkutano mwingine wa kimataifa pia kuzungumzia swala la Afghanistan kufanyika huko The Hague. Mwanadiplomsia mkuu wa Marekani Hillary Clinton na ujumbe kutoka Iran, watahudhuria.

Taarifa kutoka Washington zinasema Rais Barack Obama atatangaza rasmi leo, mpango wake wa kuwatuma wanajeshi wengine 4,000 nchini Afghanistan kupambana na uasi wa kitaliban.

Jukumu kubwa la vikosi hivi vya Marekani, ni kuwapa mafunzo wanajeshi wa Afghanistan kuweza kumudu makabiliano na waasi wa kitaliban na wale wa Al- Qaeda. Marekani ina mpango wa kuliongeza jeshi la Afghanistan kutoka wanajeshi 80,000 hadi laki moja na nusu. Hii itakuwa mara ya pili wa rais Obama kutuma vikosi vya Marekani Afghanistan, kwani tayari alikuwa ameagiza wanajeshi 17,000 kuelekea Afghanistan kujaribu kuzima uasi uliokuwa umezidi nchini humo.


Kabla ya taarifa rasmi kutoka kwa Obama, maafisa wakuu wa utawala wake walitangaza kuwa Washington itajumuisha mataifa jirani, kama vile Urusi, China, India na hata Iran , bila kusahau Pakistan katika mapambano haya ya kuwamaliza waasi wa kitaliban.


Obama ambaye alimshtumu mtangulizi wake rais George Bush kwa kushughulikia tu Iraq na kuacha mambo yaharibike Afghanistan, aliagiza kugeuzwa kwa sera, mara moja tu alipoingia madarakani mapema mwaka huu.


Usalama wa Afghanistan pia ndio ajenda katika mkutano mwingine wa kimataifa mjini Moscow. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki -Moon ni miongoni wa wale wanaohudhuria mkutano wa kuzungumzia ulanguzi wa dawa za kulevya na swala la usalama Afghanistan. Mwenyeji wa mkutano huo Urusi walisema wako tayari kushirikiana na jumuiya ya kujihami ya NATO kupata suluhu Afghanistan.


China na mataifa mengine ya bara Asia pia yanahudhuria mkutano huo. Haya yote yanafanyika siku nne tu kabla ya ule mkutano wa kimataifa pia kuzungumzia swala la Afghanistan, utakaondaliwa The Hague. Mkutano huo utakaohudhuriwa na mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Hillary Clinton, utagonga vichwa vya habari hasa baada ya Iran kusema itahudhuria pia. Wizara ya mambo ya nje, nchini Iran, imesema Tehran itakuweko The Hague kushiriki . Hata hivyo Washington imesema hakuna mpango wowote kwa Clinton kufanya mazungumzo ya pembeni na ujumbe kutoka Iran.


Kuhudhuria kwa Tehran, kunafungua ukurasa mpya, kinyume na ilivyokuwa katika enzi ya rais George Bush. Iran ilisusia mkutano mwingine kama huu mwaka jana wakati Bush alikuwa rais. Mapema mwezi huu Hillary Clinton alitoa mualiko kwa Tehran kujiunga na mataifa mengine, yanayosemekana ni muhimu kusaidia kupata amani Afghanistan.


Tangu kuingia madarakani Obama ameionyeshea mkono Iran, msimamo tofauti na mtangulizi wake Bush aliyeijumuisha Tehran kama yale mataifa maovu duniani. Kilele cha sera hii mpya ilikuwa wiki jana pale Obama kupitia ukanda wa video alisema Marekani iko tayari kuipokea Tehran kuchukua nafasi yake muhimu katika jumuiya ya mataifa. Washington na Tehran zilikatiza uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka wa 1980.


Mwandishi : Munira Muhammad/ AFP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 27.03.2009
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HKhl
 • Tarehe 27.03.2009
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HKhl
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com