Obama atarajia kutamba mbele ya Clinton huko Mississippi | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama atarajia kutamba mbele ya Clinton huko Mississippi

Iran yasema haimuungi mkono mgombea yeyote huku Indonesia ikimuombea Obama awe rais wa Marekani

default

Obama (kulia) na Clinton

Seneta Barack Obama, anapania kumshinda mpinzani wake wa chama cha Democratic, seneta Hillary Clinton, kwenye uchaguzi wa awali katika jimbo la Mississippi kutafuta uteuzi wa chama hicho kuwania urais wa Marekani wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu nchini humo.

Seneta Obama wa jimbo la Illinois ana matumaini makubwa ya kumshinda seneta Clinton wa jimbo la New York hapo kesho katika uchaguzi wa awali wa kumtafuta mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic kwenye jimbo la Mississippi.

Obama ana nafasi kubwa ya kushinda katika jimbo hilo lenye idadi kubwa ya wamarekani weusi wafuasi wa chama cha Democratic ambao wamemsaidia kushinda katika majimbo mengine. Kura za maoni zinampa ushindi Barack Obama wa pointi 24 kwa 6 katika jimbo la Mississippi.

Obama anataraji kuendeleza ushindi wake baada ya kumshinda Clinton katika uchaguzi wa awali uliofanyika mwishoni mwa juma katika jimbo la Wyoming. Ushindi huo ulimuwezesha kuendelea kuongoza kwa idadi ya wajumbe.

Seneta Obama anatarajiwa kuihutibia mikutano miwili ya hadhara hii leo huko Columbus na Jackson Mississippi, huku akijaribu kujikingia idadi kubwa ya wajumbe 33 walio katika jimbo la Mississippi, watakaopiga kura kumteua mgombea wa chama cha Democratic katika mkutano mkuu wa chama.

Hillary Clinton aliyefanya kampeni katika jimbo hilo wiki iliyopita, anapanga kufanya kampeni katika jimbo la Pennsylvania, ambako kuna idadi ya wajumbe 158 watakaoshindaniwa katika uchaguzi wa awali wa tarehe 22 mwezi ujao wa Aprili.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton ameungana na mke wake Hillary wakisema Obama, ambaye wanamueleza kuwa mwanasiasa asiye na uzoefu, anaweza kuwa mgombea mwenza wa Hillary kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Seneta John Kerry, aliyewania urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic mnamo mwaka wa 2004 na ambaye anamuunga mkono seneta Obama, amelalamika kuwa kampeni ya Clinton inadhihaki uwezo wa Obama kushindana na mgombea urais wa chama cha Republican, seneta wa jimbo la Arizona, John McCain.

Iran haimuungi mkono mgombea yeyote

Wakati huo huo, Iran imesema haimuungi mkono mgombea yeyote wa urais wa Marakeni lakini inatumai uchaguzi huo utaleta mabadiliko ya sera za kigeni za Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran mjini Tehran, Mohammed Ali Hosseini, amesema mataifa duniani yamechoshwa na sera za Marekani kueneza vita na kutaka zibadilike.

Mapema mwezi huu, rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, aliliambia gazeti la El Pais la nchini Uhispania kwamba hali ya kisiasa nchini Marekani itamruhusu seneta Obama aingie ikulu. Aidha rais huyo alisema hatakuwa na matatizo yoyote iwapo seneta huyo kijana wa jimbo la Illinois atachaguliwa kuwa rais wa Marekani.

Waindonesia wamuombea Obama ashinde

Huku mashindano ya kuwania uteuzi wa urais wa Marekani yakiwa yamepamba moto, raia wengi nchini Indonesia wanamuombea Obama ashinde urais wa Marekani wakiamini atakuwa rais shupavu.

Obama amepata umaarufu mkubwa nchini Indonesia kwa kuwa alikulia nchini humo wakati wa utoto wake na alisoma katika shule mbili za msingi mjini Jakarta katika miaka ya 1960.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Besuki, Kuwadiyano, ameliambia shirika la habari la Ujerumani, Deutsche Presse Agentur, DPA, kuwa wanajivunia mmoja wa wanafunzi wao kugombea urais wa Marekani.

Shule ya msingi ya Besuki ni shule ya serikali iliyo na sifa nzuri kimasomo na huwakubali wanafunzi kutoka matabaka mbalimbali ya kidini. Masomo yanayofunzwa yanalingana na mtalaa wa kitaifa na wanafunzi ambao si waislamu hupata mafunzo ya dini zao katika madarasa tofauti.

Obama aliyezaliwa nchini Marekani katika jimbo la Hawaii, alikwenda Indonesia akiwa na umri wa miaka sita baada ya mamake mmarekani, Ann Dunham, kuolewa na muislamu raia wa Indonesia, Lolo Soetoro, baada ya kuachana na mume wake raia wa Kenya.

Obama alisoma katika shule za Indonesia hadi alipofikia umri wa miaka 10 na kisha akarejea Hawaii kuishi na wazazi wa mamake.

 • Tarehe 10.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DLtK
 • Tarehe 10.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DLtK
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com