1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza njia za kukabiliana na nakisi kubwa

Abdu Said Mtullya14 Aprili 2011

Obama asema njia ya ufanisi ya kukabiliana na nakisi kubwa ni kupunguza matumizi ya serikali na kuongeza kodi kwa matajiri

https://p.dw.com/p/10tCh
Rais Barack Obama akitoa hotuba juu ya kupunguza nakisiPicha: dapd

Rais Obama ametangaza mpango wa kupunguza matumizi ili kukabiliana na nakisi kubwa katika bajeti ya nchi.

Akihutubia mjini Washington Obama alitoa mwito wa kuwatoza kodi zaidi matajiri pamoja na kupungua matumizi ya serikali.Lengo la hatua hizo ni kupunguza nakisi kwa kiasi cha dola Trilioni 4 mnamo kipindi cha miaka 12 ijayo.

Pamoja na hatua zingine alizopendekeza Rais Obama ni kupunguza bajeti ya ulinzi,na kuzuia ongezeko la gharama za huduma za afya. Deni la serikali ya Marekani sasa limefikia kiasi cha dola Trilioni 14.

Juu ya mapendekezo ya Rais Obama, wajumbe wa chama cha Republican wamesema kuwa hotuba ya Rais huyo ni porojo za kampeni. Wamesema mpango wowote juu ya kuongeza kodi kwa matajiri ni sawa na farasi asieweza kukimbia.

Lakini Rais Obama ameilaumu mipango ya Republican ambayo amesema itawaumiza masikini na wazee.Obama amewaambia wananchi wake kwamba Marekani inapaswa kujikuna pale inapojiweza.Amesema lazima nakisi ipunguzwe ili kuweza kurejea katika mkondo wa kupunguza deni la nchi. Lakini ameeleza kuwa hayo yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia hatua za kudumisha ustawi wa uchumi na kutenga nafasi za ajira.