Obama asema Marekani haiko vitani na Uislamu | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama asema Marekani haiko vitani na Uislamu

Rais wa Marekani Barack Obama amewataka viongozi wa nchi na wa Kiislamu kupambana na itikadi potofu za kidini zinazoenezwa na makundi ya kigaidi kama la dola la kiislamu la IS na kudhihirisha kuwa hayauwakilishi Uislamu.

Rais Obama amesema hapo jana katika mkutano wa kujadili jinsi ya kukabiliana na kitisho cha itikadi kali duniani uliowaleta pamoja wajumbe kutoka nchi sitini katika ikulu ya Rais kuwa wanamgambo wenye itikadi kali sio viongozi wa kidini bali ni magaidi.

Rais huyo wa Marekani amesisitiza kuwa Marekani haipigani dhidi ya Uislamu wala haina nia ya kuukandamiza Uislamu bali inapambana na watu wanaopotosha dini hiyo.

Uislamu haukandamizwi

Amewataka viongozi wa Kiislamu waliokuwa katika mkutano huo wa kilele kuangazia kwa dhati dhana potofu kuhusu Uislamu na dhana kuwa nchi za magharibi zinaupinga Uislamu na kuongeza hakuna dini iliyo ya kigaidi bali ni watu wanaofanya ugaidi.

Bendera ya kundi la wanamgambo wa IS

Bendera ya kundi la wanamgambo wa IS

Obama ametaka kuongezeka kwa juhudi za kushughulikia itikadi kali kwa kuzungumzia wazi vitendo vya kigaidi kwa kutumia hasa mitandao ya kijamii ambayo makundi yenye itikadi kali kama la IS yanatumia kuwasajili vijana kutokana na matatizo ya kiuchumi na kisiasa ambayo wanaitumia kuwashawishi kuwa na misimamo mikali.

Obama amezungumzia kuhusu kadi aliyopokea siku ya wapendanao iliyomgusa kutoka kwa msichana wa Kiislamu wa miaka 11 kwa jina Sabrina ambamo msichana huyo alisema ana wasiwasi kuwa watu wanawachukia Waislamu na kumtaka Rais Obama kuwaambia kila mmoja kuwa Waislamu ni watu wazuri tu kama watu wengine.

Katika mkutano tofauti katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani kujadili suala hilo hilo la kitisho cha itikadi kali, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kuuawa kwa raia 21 wa Misri wakristo nchini Libya na wanamgambo wa IS kunadhihirisha ukatili wa kundi hilo na kuongeza mauaji ya kinyama kama hayo yanawapa nguvu kukabiliana na makundi kama hayo.

Wapiganaji wa kigeni ni kitisho

Kerry amesema kiasi ya wapiganaji 20,000 wa kigeni wamesafiri kuelekea Syria na Iraq na huenda wakawa kitisho iwapo watarejea nyumbani kwa kufanya mashambulizi kama yaliyotokea Paris na Copenhagen katika wiki za hivi karibuni.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry

Mkutano huo wa kilele kuhusu usalama utakamilika hii leo ambapo mawaziri na maafisa wa nchi sitini watajadili juhudi za kupambana na wapiganaji wa kigeni na itikadi kali kwa kuangazia jinsi ya kutambua na kupunguza vichocheo vya ghasia zitokanazo na itikadi kali, kukomesha ushawishi wake, kutafuta njia za kuzipa jamii uwezo na kuhakikisha kuna fursa za kiuchumi kwa makundi ya watu walio katika hatari ya kushawishika kujiunga na makundi ya itikadi kali.

Mawaziri watajadili pia ushirikiano ukiwemo kufuatilia nyendo za wapiganaji wa kigeni kupitia uchunguzi katika viwanja vya ndege na kubadilishana taarifa za kiusalama.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com