Obama amezuru Hiroshima | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama amezuru Hiroshima

Obama amekuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyeko madarakani kuzuru eneo la mji wa Hiroshima ambalo Marekani ilishambulia kwa kutumia bomu la kwanza la atomiki mwaka 1945 na kuua takriban watu 140,000.

Obama akiweka shada ya maua Hiroshima.

Obama akiweka shada ya maua Hiroshima.

Baada ya kuweka shada ya maua katika bustani ya amani eneo la Hiroshima-Japan, rais Obama alitoa hotuba ya kumbukumbu ya mashambulizi hayo ya Hiroshima huku akisisitiza matumaini kuwa uhusiano kati ya Japan na Marekani utazidisha matumaini katika juhudi za kutupilia mbali matumizi ya silaha za atomiki.

Obama amekuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyeko madarakani kuzuru eneo la mji wa Hiroshima ambalo Marekani ilishambulia kwa kutumia bomu la kwanza la atomiki mwaka 1945 na kuua takriban watu 140,000. Obama amefanya ziara hiyo ya kihistoria baada ya mkutano wa viongozi wa nchi saba tajiri kiviwanda duniani ambapo viongzo hao wamekubali kuimarisha uchumi wa dunia.

Upatanisho

Anayesikitikia shambulizi la Hiroshima.

Anayesikitikia shambulizi la Hiroshima.

Shambulizi la bomu la kwanza la atomiki eneo la Hiroshima mwaka 1945 na pia Nagasaki lilisababisha vifo maelfu ya watu papo hapo, na baadaye jumla ya watu 140,000 walifariki. Japo hakuomba msamaha jinsi Ikulu ya White House ilivyotangaza awali, Obama amesikitikia waliopoteza uhai wao miaka 71 iliyopita kufuatia mashambulizi hayo yaliyoifanya Japan kusalimu amri na hivyo vita vikuu vya pili vikakamalizika.

Waziri mkuu wa Japan Abe Shinzo ambaye ni mwenyeji wa Obama amesema, ziara ya Obama katika bustani ya Hiroshima inafungua ukurasa mpya wa upatanisho baina ya mataifa hayo mawili

Ziara ya Obama inajiri wakati viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda wakikubaliana kuwa haja ya kuimarisha uchumi wa dunia inapaswa kupewa kipaumbele ya dharura. Viongozi hao pia wameonya kuwa huenda kukatokea athari kubwa ikiwa Uingereza itapiga kura ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, katika kura ya maamuzi inayotarajiwa mwezi ujao. Mkutano huo wa siku mbili uliofanywa mji wa Ise-Shima Japan umekamilika.

Mwandishi: John Juma/ AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com