Obama akutana na viongozi wa ghuba | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama akutana na viongozi wa ghuba

Rais Barack Obama wa Marekani amekuwa na mazungumzo leo(21.04.2016)na viongozi wa mataifa ya ghuba nchini Saudi Arabia ili kuhimiza kampeni kali zaidi dhidi ya kundi la IS.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad

Mkutano wa kundi la GCC nchini Saudi Arabia pamoja na rais Obama wa Marekani

Rais Barack Obama anafanya mazungumzo hayo licha ya mahusiano yaliyoingia doa kati ya nchi hizo na Marekani.

Mikutano hiyo mjini Riyadh leo ililenga katika kujenga mwendelezo wa mikutano kama hiyo iliyoitishwa mwaka jana Camp David, eneo la mapumziko ya rais wa marekani katika jimbo la Maryland.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad

Rais Barack Obama akizungumza na mfalme wa Saudia ,Salman.

Mikutano hiyo inaakisi juhudi zinazochukuliwa na Ikulu ya Marekani kuwahakikishia na kufanya uratibu na washirika wake wa mashariki ya kati ambao ni muhimu lakini wenye shaka shaka ambao wanapinga mjongeleano wa Obama na Iran pamoja na sera za Marekani kuelekea vita nchini Syria.

Mkutano na nchi washirika wa Marekani wa baraza la ushirikiano la mataifa ya ghuba unafuatia mazungumzo ambayo Obama alifanya na mfalme wa Saudia, Salman jana muda mfupi baada ya kuwasili katika nchi hiyo ya kifalme.

Mbali na Saudi Arabia , nchi hizo za GCC ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain.

Marekani na Iran

Uungaji mkono wa Marekani katika kuondoa vikwazo dhidi ya Iran baada ya makubaliano ya mwaka jana ya kinyuklia yameuweka katika majaribu uhusiano kati ya Marekani na baraza hilo la mataifa ya ghuba likiongozwa na Saudi Arabia.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad

Rais Obama akishiriki katika mkutano wa baraza la ushirikiano la mataifa ya ghuba mjini Riyadh

Viongozi hao wamejadili pamoja na mambo mengine mizozo ya kikanda nchini Syria , Iraq na Libya pamoja na njia za kuimarisha mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Wasi wasi wa mataifa ya ghuba

Ikulu ya Marekani imesema mkutano huo utajumuisha vikao vitatu. Cha kwanza ni kuimarisha uthabiti wa kikanda na kingine kitahusu juhudi za kupambana na ugaidi ikiwa ni pamoja na juhudi za kuliangamiza kundi la al-Qaeda na wanamgambo wa Dola la Kiislamu.

Saudi Arabia, falme za Kiarabu na mataifa mengine ya ghuba yanakubaliana na mtazamo kwamba wanamgambo wa IS ni kitisho, na wamejiunga na kampeni inayoongozwa na Marekani ya kulishambulia kundi hilo. Lakini wanataka Marekani kufanya zaidi kujaribu kumuondoa madarakani rais wa Syria Bashar al Assad.

Saudi-Arabien König Salman empängt Barack Obama

Mfalme Salman akimkaribisha rais Obama katika ukumbi wa mkutano.

Mataifa ya ghuba pia yana shaka kubwa kuhusiana na utayari wa Obama kuweza kujadiliana na Iran taifa la Kishia lenye nguvu, na zinahofia kwamba makubaliano ya mwaka jana ya kinyuklia na jamhuri hiyo ya Kiislamu yataelekeza katika kuweka uwiano mpya wa misimamo ya kikanda na kuzigharimu nchi hizo.

Mataifa kadhaa ya ghuba yanayoongozwa na Wasunni yanaona uungaji mkono wa wanamgambo wa Kishia nchini Lebanon, Yemen na Iraq kuwa sababu kubwa ya kuwapo kwa mvutano wa kimadhehebu na kutokuwa na uthabiti katika kanda hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe , ape, dpae

Mhariri: Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com