Obama aisihi India kuwa na uvumilivu wa kidini | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama aisihi India kuwa na uvumilivu wa kidini

Rais Barack Obama wa Marekani ameionya India haitofanikiwa iwapo itaendelea kugawanyika katika misingi ya kidini, huku akiitaka pia nchi hiyo kuzingatia haki za wanawake na umuhimu wa kutoa fursa sawa kwa kila mtoto.

Rais Barack Obama akiwahutubia watu wa India 27.01.015

Rais Barack Obama akiwahutubia watu wa India 27.01.015

Rais Obama ameyatoa matamshi hayo hii leo mjini New Delhi, mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu nchini India. Akizungumza na umati wa kiasi cha watu 2,000 wengi wao wakiwa ni vijana, Rais Obama amesema kila mtu anapaswa kufuata imani ya dini yake bila ya kuwa na hofu ya kuteswa, akikumbushia kwamba Katiba ya India nchi yenye Wahindu wengi ina kipengele kinachoelezea uhuru wa dini.

''Tumeona dunia ikikabiliwa na hali ya kutovumiliana na ghasia na ugaidi unaofanywa na wale wanaodai kuwa wanasimamia imani yao, lakini ukweli ni kwamba wanaisaliti. Mara nyingi dini imekuwa ikitumika kufanya maovu, ambayo ni kinyume kabisa na nuru ya Mungu'', alisema Obama.

Rais Obama akiwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi

Rais Obama akiwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi

India ni nchi isiyofungamana na dini, lakini historia yake inaonesha kukumbwa na mizozo ya kidini, hasa dhidi ya jamii chache ya Waislamu. Rais Obama amesema India itaendelea ikiwa haitogawanyika katika misingi ya kidini, hivyo inapaswa kuwa na uvumilivu wa kidini.

Suala la uhuru wa dini limekuwa likizusha utata hasa tangu ulipofanyika uchaguzi wa mwaka uliopita uliompa ushindi Waziri Mkuu Narendra Modi, wa chama cha Wazalendo wa Kihindu.

Obama asisitiza kuhusu haki ya mwanamke

Aidha, Rais Obama alisisitiza kuhusu hadhi ya mwanamke katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Kailash Satyarthi. Amesema dunia itakuwa imara iwapo haki ya mwanamke itazingatiwa, wakiwemo wanawake wa India. Pia alizungumzia namna India ilivyowaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini na jinsi India na Marekani zinavyowasaidia watu kupata fursa.

Rais Obama akisalimiana na umati wa watu waliokuwa wakimsikiliza

Rais Obama akisalimiana na umati wa watu waliokuwa wakimsikiliza

Ama kwa upande mwingine Rais Obama amesema Marekani inaweza ikawa mshirika mzuri wa kibiashara wa India, huku akiitaka India kuchukua hatua zaidi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Amesema India ndiyo inapaswa kufanya maamuzi kuhusu jukumu lake duniani na kujielekeza katika ushirika muhimu kwenye karne ya sasa.

Amesema anaamini kwamba watu wa nchi hizo mbili watapata ajira na fursa zaidi, hivyo kuyafanya mataifa hayo kuwa salama zaidi na dunia kuwa eneo salama na lenye kuzingatia haki, iwapo demokrasia ya nchi hizo mbili zitakuwa na msimamo mmoja.

Obama ambaye alikuwa Mgeni wa Heshima katika sherehe za Siku ya Jamhuri, hapo jana, baadae leo ataelekea nchini Saudi Arabia kutoa rambirambi zake kwa Mfalme mpya wa nchi hiyo, Salman, kutokana ya kifo cha Mfalme Abdullah, kilichotokea wiki iliyopita. Rais Obama ataongozana na ujumbe wa watu 30, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com