Obama aipa changamoto Kenya kuhusu haki za mashoga na rushwa | Matukio ya Afrika | DW | 26.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Obama aipa changamoto Kenya kuhusu haki za mashoga na rushwa

Rais wa Marekani Barack Obama anakamilisha ziara ya kihistoria ya siku mbili nchini Kenya leo (26.07.2015) ambako atalihutubia taifa hilo kabla ya kuelekea nchini Ethiopia.

Barack Obama in Kenia mit Präsident Uhuru Kenyatta bei gemeinsamer Konferenz in Nairobi

Rais Barack Obama na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta wa Kenya

Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari baada ya mazungumzo yao na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Obama amelinganisha chuki dhidi ya watu wanaofanya mapenzi kwa jinsia moja inayoongezeka barani Afrika na ubaguzi wa rangi aliokumbana nao nchini Marekani.

Baada ya kuahidi ushirikiano imara wa biashara na misaada kwa wajisiriamali, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kupambana na rushwa iliyokithiri, akiita kuwa ni kikwazo cha kwanza kikubwa katika ukuaji wa haraka wa uchumi wa Kenya.

Barack Obama in Kenia mit Präsident Uhuru Kenyatta

Barack Obama akikutana na Uhuru Kenyatta

Obama aliwasili nchini Kenya Ijumaa jioni(24.07.2015) akifanya ziara yake ya kwanza akiwa rais wa Marekani katika nchi hiyo ambayo baba yake alizaliwa na ya kwanza katika taifa hilo la Afrika mashariki akiwa rais wa Marekani aliyeko madarakani.

Obama kuhutubia taifa Kenya

Leo Jumapili(26.07.2015) rais Obama anatarajiwa kulihutubia taifa la Kenya na kukutana na wajumbe wa vyama vya kijamii nchini Kenya.

Ataondoka baadaye leo jioni kwenda katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, ambako pia atakuwa rais wa kwanza wa Marekani kuhutubia Umoja wa Afrika.

Ethiopia imetoka mbali kuanzia kuwamo katika vichwa vya habari mara nyingi duniani katika mwaka 1984 kutokana na njaa, hadi kufikia ukuaji wa uchumi wa karibu asilimia kumi na uwekezaji mkubwa katika miundo mbinu na kuifanya nchi hiyo kuwa moja kati ya nchi za juu kabisa katika bara la Afrika zinazofanya vizuri katika uchumi na hivyo kuwa kivutio kikubwa cha wawekezaji wa nje.

Barack Obamas Präsenz in Nairobi Kenia findet große Beachtung

Watu wengi walijitokeza kumlaki Obama nchini Kenya

Taifa hilo la pembe ya Afrika pia linabaki kuwa kivutio kwa wafadhili wa kimataifa, licha ya kuwepo wasiwasi kuhusiana na haki za binadamu, na kuwa kitovu cha utulivu katika eneo ambalo kwa kawaida lina matatizo.

Obama kuhutubia viongozi wa Umoja wa Afrika

Obama anatarajiwa kuwahutubia viongozi katika makao makuu ya Umoja wa Afrika wakati akikamilisha ziara yake ya Afrika siku ya Jumanne, kwa matamshi ambayo huenda yakagusia upungufu wa demokrasia katika bara la Afrika.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, amesema "itakuwa ziara ya kihistoria" na itakuwa "hatua muhimu kupanua na kuimarisha uhusiano kati ya Umoja wa Afrika na Marekani."

Nkosazana Dlamini-Zuma

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma

Obama pia anatarajiwa kukutana na wapatanishi wanaoendesha juhudi za kusaka amani katika nchi jirani ya Sudan Kusini, taifa changa kabisa duniani, ambalo limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu sasa miezi 19.

Wakati Kenya imefanya operesheni kubwa kabisa ya usalama kuwahi kuonekana katika mji mkuu Nairobi kwa ajili ya Obama, ulinzi mkubwa wa wanajeshi nchini Ethiopia una maana kwamba hakutakuwa na hali ya sherehe wakati wa kuwasili kwa rais huyo wa Marekani.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe

Mhariri: Elizabeth Shoo